Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mjadala kuhusu wazo la fikra jumuiya (collective thinking) na mchango wake katika kuhimiza umoja, usalama na maendeleo ya nchi. Wazo hili limezua mjadala kwa kuwa kuna baadhi ya watu wanaona kuwa nchi yetu inapungukiwa kitu fulani, kwa hiyo inatakiwa kuwa na kitu hicho ili tujue tunaelekea wapi. Baadhi wanaona wazo hili si jambo halisi, linaongeleka tu lakini haliwezi kutekelezwa, kwa kuwa wanaona si rahisi kwa kundi kubwa la watu kufikiri kwa njia moja au kuwa na ndoto moja. Lakini wengine wanaona kuwa wazo hili ni jambo halisi na ni msingi wa mwongozo wa maendeleo ya nchi.
Ili kujua kama kweli wazo hili ni jambo la kufikirika tu au ni jambo halisi, ni vizuri tukijaribu kuziangalia nchi kwa kutumia mfano wa binadamu. Kwa kawaida kwa mtu anayeishi kwa kuangalia mbali, kujiwekea malengo na mipango ya kufikia malengo hayo, huwa ana mafanikio katika maisha yake. Lakini mtu anayeishi kwa mtindo wa kuzingatia mambo ya leo tu, na kukabiliana na changamoto za leo za kesho anamwachia Mungu, mara nyingi maisha yake yanakosa mwelekeo, leo anaweza kuwa na neema kubwa na kesho akawa na taabu kubwa, na mara nyingi mwisho wake unakuwa mbaya. Wachina wana methali moja inayosema usipoangalia mbali, taabu inakukaribia.
Kuna wakati nchi huwa zinakuwa na tabia kama za binadamu, zinafikiria, kupanga na kutekeleza mipango yake. Lakini kama ilivyo kwa binadamu, kuna baadhi ya nchi zinaonekana wazi kabisa kuwa na ndoto, na zinaonekana wazi kabisa jinsi zinavyofanya kazi kutimiza ya ndoto hizo. Nchi za namna hiyo kimsingi zinakuwa imara na zinapiga hatua. Lakini kuna nchi nyingine hazionekani kama zina ndoto au kuwa na mipango yoyote halisi ya kuendeleza nchi, au hata kufikiri nchi hiyo itakuwa na sura gani katika miaka 20 au hata 50 ijayo, ni kama zinaishi na kusibiri jua lichomoze na kuzama. Hazina ndoto ya kutaka siku moja ziwe nchi za namna gani. Nchi kama hizo hazitabiriki, kuna wakati zinakumbwa na majanga yasiyofikirika, na hata kuleta matatizo makubwa kwa nchi au jumuiya nyingine.
Kabla ya kujiangalia sisi watanzania tuko wapi, ni vizuri tuangalie nchi zilizojitangaza wazi kuwa zina ndoto ziko wapi na zinafanya nini katika kutimiza ndoto hizo. Katika siku za hivi karibuni China imekuwa ikitangaza kuhusu “ndoto ya China”. Kimsingi ndoto ya China inahusu nia ya wachina ya kuona nchi yao inakuwa na neema, na neema hiyo itatokana na wachina wenyewe kufanya juhudi kwa pamoja, kwa kufuata ujamaa unaolingana na hali halisi ya China. Kama nchi ikiwa na neema na ustawi, watu wake wanakuwa na neema. Ukiangalia maendeleo ya uchumi na jamii ya China kwa sasa, unaweza kuona wazi kabisa kuwa wachina wanafanya kazi, na wanaelekea kutimiza ndoto yao. Ukijaribu kuchambua kwa undani ndoto hii, kwa ufupi unaweza kuona kuwa inaeleza ni nini wachina kwa ujumla wao wanafikiri na kukifanya kwa ajili ya kuendeleza nchi yao.
Wamarekani pia wana ndoto yao American dream, wao wanaona kuwa nchi yao itakuwa na neema na nguvu kama watu wanaoishi katika nchi yao, bila kujali wanatoka wapi, wanaonekana vipi au wana imani gani, wanakuwa na fursa ya kuwa na neema na mafanikio. Kwa hiyo wamejitahidi kuweka mazingira ya haki ambayo mtu yoyote akifanya juhudi basi atakuwa na neema na mafanikio anayostahili. Na kama watu wakiwa na neema na mafanikio basi nchi yao pia itakuwa na neema na mafanikio.
Wazo la ndoto ya nchi ni suala la fikra jumuiya (collective thinking) Wazo hili linaweza kuonekana kuwa ni wazo la kufikirika tu (utopian) kwa kuwa labda watu wengi wenye hali tofauti, kama vile viwango vya elimu, mawazo, mazingira ya kuishi na upeo wao, hawawezi kufikiri kwa njia moja. Lakini tukiangalia hali halisi katika nchi ambazo zimetamka wazi kuhusu jambo hili na kulifanyia kazi, wazo hili linaonekana wazi kuwa ni kitu halisi, na linaweza kutekelezeka.
Sisi watanzania kwa ujumla wetu tunatakiwa kujiuliza na kujua, ndoto yetu ni ipi? Tunataka kuipeleka wapi Tanzania? na vipi tunaipeleka Tanzania tunakotaka iende? Kwa sasa ni vigumu sana kupata majibu ya maswali haya. Wakati wa enzi za awamu ya kwanza tulikuwa na kitu kinachofanana na “ndoto ya Tanzania”, yaani kuijenga Tanzania kuwa nchi “ujamaa na kujitegemea”, ambayo wananchi wake wanaishi kwa haki, usawa na neema. Pamoja na kuwa ndoto hiyo ambayo ilitangazwa kuwa sera ya nchi ilikuwa inapingwa, ilieleza vizuri maana ya ujamaa na kujitegemea na kueleza wazi nini kinafanyika ili kujenga nchi ya ujamaa inayojitegemea, na hayo yalikuwa yanaonekana.
Mwaka 1992 tulipoanza kutekeleza mageuzi ya kimuundo (structural adjustment programmes), tuliyotakiwa kuyatekeleza na Shirika la fedha la Kimataifa IMF, ilionekana wazi kabisa kuwa ndoto yetu ilifutika. Tatizo ni kwamba baada ya kuondoa sera ya ujamaa na kujitegemea, hatukuleta kitu mbadala ambacho kinaeleza wazi kuwa tunajenga nchi ya namna gani. Mpango wa maendeleo ya Tanzania kuelekea mwaka 2025 (Vision 2025) uliotangazwa kama mbadala wa sera hiyo, ni dira tu inayotuongoza kwenda mwaka 2025, inaishia hapo tu haielezi Tanzania itaenda wapi baada ya hapo, lakini Tanzania na watanzania wataendelea kuwepo hata baada ya hapo.
Mwanataaluma mmoja wa Tanzania Dr Malima Bundala aliandika kitabu kinachotoa changamoto kubwa kwa watanzania kuhusu fikra jumuiya. Dr Bundala anaona kuwa jamii bila kuwa na fikra jumuiya, ni vigumu sana kwa jumuiya hiyo kupata maendeleo, au kuwa mwelekeo unaoeleweka. Kwa sasa sisi watanzania tunaonekana kuwa na udhaifu kwenye jambo hilo. Japo kuwa tunajidai na kujitangaza kuwa sisi ni watanzania, kimsingi tunaonekana kuwa tumeisahau kabisa Tanzania yenyewe. Inawezekana kuwa leo ukimuuliza mwanaCCM atakwambia “ndoto yangu ni kuona chama changu kinaendelea kutawala”, ukimuuliza mtu wa upinzani jibu litakuwa ndoto yangu kubwa ni kuiondoa CCM madarakani. Tunayojali zaidi ni mambo binafsi na jumuiya zetu ndogo ndogo, Tanzania tumeiweka mwisho kabisa.
Wakati umefika tukumbushane kuwa sisi ni watanzania na tunahitaji ndoto ya namna moja ya kitanzania, ambayo inaweza kutukumbusha tulikotoka, tulipo na tunakotaka kuelekea. Kana tukiendelea na mtindo wa kutoangalia mbali, basi mbeleni tuna hatari kubwa.