Quantcast
Channel: Uchambuzi – FikraPevu
Viewing all 186 articles
Browse latest View live

Mtwara: Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi!

$
0
0

Kwa wiki ya tatu mfululizo kumekuwa na malumbano kuhusiana na suala la ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Kumekuwa na madai yenye nguvu ya hoja kutoka kwa wananchi wa Mtwara dhidi ya porojo kutoka kwa viongozi wenye dhamana ya kujibu madai haya ya watu wa Mtwara.

Watu wa Mtwara kwa umoja wao na kwa kuungwa mkono na viongozi wa dini zote wamekuwa wakitaka Serikali ifikirie upya suala la mradi wa ujenzi wa Bomba la gesi na badala yake kujenga mitambo ya kufua umeme mkoani Mtwara na kusafirisha umeme huo kwenda maeneo mengine ya nchi. Kwenye moja ya maandishi yangu (Serikali iwasikilize watu wa Mtwara) nimeshauri kuwa Taifa liwe na gridi nyingine ya Taifa ambayo itatokana na Gesi tu na ianzie Mtwara.

Ikumbukwe kwamba, katiba ya nchi ibara ya 9 katika mabano J inataka mamlaka ya dola na vyombo vyake vyote kuhakikisha ya kwamba shughuli zote za kiuchumi zinaendeshwa kwa namna ya kwamba pasiwe mrundikano wa utajiri au shughuli za uzalishaji kwa watu wa chache. Katiba inaendela kwa kuelekeza kwamba uchumi wa nchi upangwe katika uwiano sawia (9, d). Watu wa Mtwara wanatekeleza matakwa haya ya katiba kwa kukataa mrundikano wa shughuli za kiuchumi wa nchi na utajiri wa nchi kua kwenye mikoa michache na hasa mkoa wa Dar-Es-Saalam.

Serikali imekuwa ikitoa majibu ya porojo na kuwatusi watu wa Mtwara na kama ilivyozoeleka Rais Jakaya Kikwete na Mawaziri wake wamekuwa wakisema suala la Mtwara linatumika na wanasiasa kujitafutia umaarufu. Inasikitisha sana kuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwaambia mabalozi wa nchi za kigeni waliopo hapa nchini kuwa yanayoendelea mkoani Mtwara yanachochewa na Wanasiasa tuliosimama na wananchi wanaodai haki ya kufaidi utajiri wa nchi yetu. Rais Kikwete na Mawaziri wake wameshindwa kabisa kuonyesha uongozi katika suala hili na hatimaye kuhatarisha umoja wa kitaifa.

maandamano

Kwa udhaifu wa serikali na tabia ya kutafuta mchawi badala ya kutatua tatizo la msingi, wananchi wameendelea kukutana na hata wengine sasa kuanza kusambaza ujumbe wa kukata kipande cha nchi na kuanzisha Jamhuri ya Kusini. Nimeona kwenye mabango ya mkutano wa hadhara uliofanyika 19/1/2013 wananchi wakibeba mabango yanayoaishiria kuchoka kuwa sehemu ya Tanzania na kuanzisha Jamhuri ya Makonde kuanzia jiwe la Mzungu wilayani Kilwa mpaka mto Ruvuma. Haya yanatoka na kiburi cha Serikali kujishusha na kuwasikiliza wananchi wanaodai haki yao ya kikatiba.

Ni Serikali iliyokosa uhalali wa kutawala inayoweza kudharau hisia hizi za wananchi. Serikali ielewe kwamba kamwe haitaweza kulinda kila nchi ya bomba hili iwapo italijenga kwa nguvu. Badala ya kuzungumza na vyombo vya habari Serikali ifanye mazungumzo na wananchi wa Mtwara na kukubaliana na matakwa yao. Kitendo cha Serikali kung’ang’ania msimamo wake dhidi ya watu wa Mtwara ni kitendo kinachoweza kuipasua nchi na hivyo kwenda kinyume na masharti ya katiba ibara ya 28 ambayo inasema: “Kila raia ana wajibu wa kulinda uhuru wa nchi, uhuru mamlaka na umoja wa taifa.” (Ibara ya 28, 1)

Inawezekana Serikali inaogopa kuvunja makubaliano na Wachina ya mkopo wa dola za kimarekani 1.2 bilioni ambao imeuingia bila hata kushirikisha Bunge. Inawezekana pia Serikali na hasa watendaji wa Serikali waliojadili mkopo huu ‘wameshapata chao’ na hivyo kuogopa kusikiliza madai halali ya wananchi. Lakini yote hayo hayawezi kuwa zaidi ya Umoja wa nchi yetu. Hatuwezi kukubali nchi yetu ipasuke vipande vipande kwa sababu tu ya kulinda mkataba wa bilioni 1.2 tuliokopa China, ambayo serikali inang’ang’ania.

Tunafahamu kwamba ubalozi wa China umeandika barua serikalini kuwaondoa raia wa China waliopo Mtwara kwa hofu ya maisha yao. Serikali inaficha ukweli huu kama ilivyoficha ukweli kwamba Naibu Waziri wa Nishati na Madini bwana George Simbachawene alifukuzwa na wananchi wa Mtwara alipokwenda hivi majuzi. Serikali itaficha ukweli mpaka lini? Lazima tupate majawabu!

Kwanza Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa Bomba hili. Kamati ya Bunge ya POAC ilipokuwa inapitia mahesabu ya TPDC iliomba mkataba na kwa mshangao mkubwa wabunge wakaambiwa Mkataba haupo TPDC bali upo Wizarani! Kwanini Mkataba huu wa matrilioni ya Fedha unafichwa? Mkataba huu ulisainiwa pamoja mikataba mingine miwili, mmoja wa kujenga nyumba za wanajeshi wa thamani ya dola za kimarekani 400 milioni na mwingine wa mawasiliano jeshini wa dola za kimarekani 110 milioni, na mikataba yote mitatu imesainiwa kimya kimya bila kushirikisha wananchi kupitia Bunge. Lazima mikataba yote hii iwekwe wazi!

Pili, Mkataba huu uchunguzwe kama unalingana na thamani ya fedha maana kwa utafiti wa awali inaonyesha kuwa bei ya ujenzi wa bomba imepandishwa maradufu. Wastani wa kujenga bomba la gesi duniani ni dola za kimarekani 1.2 milioni kwa maili moja. Mradi huu wa Tanzania utagharimu dola za kimarekani 2.2 milioni kwa kilomita moja (maili 1 ni sawa na kilomita 1.6).

Tatu, Serikali ibadilishe Mkataba huu kuwa wa mkopo wa kujenga Mitambo ya kufua umeme Mtwara na ujenzi wa Msongo wa Umeme kama gridi ya pili ya Taifa. Kwa sasa Tanzania ina gridi moja ambayo inabebwa na bwawa la Mtera linalotegemea mto Ruaha ambao hivi sasa unakauka miezi 5 katika miezi 12 ya mwaka. Ni dhahiri kwamba kwa usalama wa Taifa na hata kwa gharama Nchi itafaidika zaidi kwa kujenga gridi nyingine kutokea Mtwara badala ya kusafirisha gesi kuja Dar-Es-Salaam.

Serikali haitashinda vita hii kwa kuzusha kwamba ama wanasiasa wanaopinga wanatumika na makampuni mengine au kwa mataifa ya magharibi kutaka kuvuruga nchi. Serikali ijitazame yenyewe. Bila kufanya hayo tunayopendekeza hapo juu, wananchi wataendelea kupigania haki yao. Hii ni vita ya uwajibikaji! Wananchi wanataka kufaidika na rasilimali za nchi yao. Kwa vyovyote vile upande wa wananchi utashinda. Vita ya uwajibikaji kwenye rasilimali za nchi sio ya vyama vya siasa, ni vita ya wananchi. Chama cha siasa kitakachokwenda kinyume na matakwa ya wananchi, kinajichimbia kaburi.


Viongozi wetu wanataka wakumbukwe kwa yepi?

$
0
0

Kila mara niangaliapo jinsi mambo yanavyoendeshwa na walio kwenye madaraka ya umma na hasa katika serikali za hivi karibuni kuna jambo ninaloliona haliko sawa. Nafahamu ili uweze kufanya kazi yako vizuri iwe katika ofisi za umma au binafsi lazima uwe na ari na hamasa ya kuifanya hiyo kazi ili iwe na matokeo mazuri na mwisho wa siku tuwe na hayo maendeleo tunayoyataka.

Historia inatufundisha jinsi baadhi ya watu waliopata kuwa viongozi kwenye nchi nyingine  walivyoweza kufanya makubwa na kuacha majina yao mioyoni mwa watu waliokuwa wakiwaongoza “legacy”. Kwangu mimi, kiongozi lazima uhamasishwe na kuiacha hiyo legacy ili watu wakukumbuke hata baada ya kutoka uongozini na hata baada ya kutangulia mbele za haki (kufa).

Kwa bahati mbaya wengi wa watu wetu katika uongozi suala hilo haliwapi motisha. Watu hawa wanapenda vyeo “ubwana mkubwa”, na vitu vingine viendanavyo na ubwana mkubwa mathalani magari mazuri. Pia nyakati zingine kupata fursa za kusukuma masuala yao ya kujinufaisha binafsi (biashara; halali na zisizo halali) kwa kutumia hizo nafasi kupata hili au lile kinyume na utaratibu. Ukisoma historia za nchi za wenzetu na hata ya kwetu kwa wakati fulani kulikuwa na watu wenye hamasa hiyo mfano; Mwalimu Nyerere, kina Bibi Titi au Edward Sokoine ambao bado wanaishi kwenye mioyo ya watanzania.

Kwa nchi za wenzetu zinazopiga hatua kubwa za kimaendeleo, viongozi wao walikuwa na ari ya kufanya makubwa kwenye nchi na kuacha majina mazuri kwenye utendaji wao kwa mataifa na serikali wanazoziongoza. Watu kama Mahathir Mohamed (waziri mkuu wa zamani wa Malaysia), Lee Kuan Yew (ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Singapore) bado wanaishi kwenye mioyo ya watu waliokuwa wakiwaongoza kwa michango yao katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi. Watawala wetu wanajua haya lakini ni kama hawana hamu hiyo ya kukumbukwa na kuingia kwenye historia ya nchi hii! Na kama huna hamasa hiyo bali tu ya kujitajirisha wewe na familia yako, kwa kweli huna haja ya kuumiza akili yako kutafuta uongozi wa umma. Wananchi wanapaswa kuwaogopa viongozi wa namna hii. Wanapaswa kuwakataa na kutokuwapa ridhaa!

Tatizo kubwa linalosababisha ukosefu wa hamasa ya ikiwemo ya mambo ya msingi kama kupiga vita umaskini au kupambana na rushwa ambayo ni matatizo yanayoikwamisha nchi yetu kupiga hatua kimaendeleo ni kutokuwa na mipango na fikra za kutizama masuala kwa muda mrefu. Wengi wa watawala wetu kutokana na matendo yao yanasanifu zaidi fikra zao kuwa katika vipindi vifupi vifupi kwa uwepo wao madarakani (kadiri ya vipindi vya kiuchaguzi). Hawataki kufikiria na kutizama taifa katika muda mrefu  hata baada ya wao kuondoka madarakani muda mrefu baadaye kwa hiyo hawana haja na kuacha majina yao yatajike kwa sababu nzuri.

Kuondoa umaskini na kupiga vita rushwa kwa vitendo badala ya maneno matupu ya kwenye majukwaa ya kisiasa tu ndiyo ingekuwa msukumo hasa unaowapa hamasa watawala wetu kutaka nafasi serikalini. Kwa kweli Tanzania isingewasahau kwa mchango huo lakini hakuna juhudi zinazotia matumaini yaani juhudi hazilingani na ukubwa wa matatizo. Bado kuna upungufu hasa wa kiutendaji kama tukipima kwa matokeo.

Nchini Brazili rais wao wa zamani, Lula da Silva atakumbukwa sana katika kujenga uchumi wa kisasa nchini mwake na hasa kupunguza umaskini wa kutupwa kwa kuwaondoka wabrazili milioni 30 kutoka kwenye umaskini wa kutupwa. Je, viongozi hujiuliza wanataka kuwaondoa watanzania wangapi kwenye umaskini wa kutupwa labda ndani ya miaka mitano?

Brazili ni mbali lakini tuangalie waethiopia watamkumbukaje waziri mkuu wao Meles Zenawi  aliyefariki mwaka jana (2012) ambaye alisimamia ukuaji wa uchumi wa Ethiopia kwa wastani wa asilimia 11 kwa miaka saba toka mwaka 2004 mpaka 2011 (kwa mujibu wa ripoti ya shirika la fedha la kimataifa (IMF)? Mwandishi na mchumi aliyebobea Joseph E. Stiglitz aliandika kwenye kitabu chake kinachoitwa “Globalization and Its Discontents”  juu ya waziri mkuu huyo wa zamani wa Ethiopia; “Meles showed that, with the right policies in place, even a poor African country could experience sustained economic growth, (Meles ameonyesha kwa kuwa na sera nzuri hata nchi masikini ya Afrika inaweza ikapata maendeleo chanya kwenye  maendeleo ya kiuchumi- tafsiri yangu).

Nawapongeza baadhi ya watendaji na mawaziri katika awamu hii hasa baada ya mabadiliko yaliyofanyika kwa kujitahidi kubadilisha hali ya wizara wanazoziongoza na taasisi zake. Tunapaswa kutambua bado kuna kazi kubwa mbeleni. Nilipata fursa kumsikiliza waziri wa uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe wakati wa uzinduzi wa safari za treni katika mji wa Dar es Salaam; kutoka Ubungo kwenda Stesheni akasema kuhusu hatua hiyo kuwa ni “kiburi tu cha mtu masikini”. Naamini tunahitaji kiburi hicho cha kujaribu pia kwenye maeneo mengine ya kupunguza kero hapana nchini.

Kwa ujumla, uongozi ni dhamana na sio kazi tu kama kazi nyingine kwamba mwisho wa siku alimradi mkono uende kinywani. Kiongozi inabidi awe mtu anayeweza kujinasibisha na watu maskini ambao ni wengi katika nchi hii. Mara nyingi naona kama wapiga kura nyakati nyingine hatufahamu ni nini viongozi wetu tunatakata watufanyie na namna gani wasipoenenda tuwawajibishe, ndiyo maana tunavumilia tu utendaji mbovu.

Ili mtu awe kiongozi lazima awe na hamasa ya kuleta mabadiliko na awe na hamasa ya kuacha jina zuri nyuma yake. Lazima awe mtu mwenye maono ya mbali, uelewa wa kutosha wa jamii hii ya watanzania anayefahamu matatizo ya watanzania na kama aliwahi kuwa kwenye uongozi basi angalau tujue aliwahi kufanya nini kwenye uongozi wake kabla labda hatujamchagua kuwa mbunge au rais.

Kinachosikitisha haionekani hamasa ninayoijadili katika nyuso na juhudi za wengi wanaoutaka urais wa mwaka 2015; naona uroho wa madaraka! Wataka uongozi wengi  hawatuonyeshi uongozi sasa! Watuonyeshe uongozi sasa kabla ya kuanza hizo mbio zao. Haiwezekani watu watumie muda mwingi kutafuta uongozi kana kwamba hiyo ni shughuli ya kudumu na pamoja na kuwa wako kwenye uongozi wa aina fulani, tayari badala ya kutumia muda huo kuonyesha uongozi washaanza kuwazia madaraka zaidi! Tumeshashuhudia baadhi ya viongozi walioenda na njia ya kutumia nguvu na mikakati mingi kupata madaraka na namna walivyoshindwa kuibadilisha nchi. Hivyo hatupaswi kuingia katika mtego ule ule.

Soko la Hisa la Dar: Fursa ya kipekee kwa wajasiriamali wazalendo Tanzania

$
0
0

Soko letu limekuwa likiwanufaisha zaidi wageni na wananchi wa nchi jirani ambao hulitumia kikamilifu kujinufaisha na wazalendo wengi kutoelewa nini kinachoendelea. Kwa wale waliokwisha jitosa, huwezi amaini jinsi wanavonufaika na kuwekeza zaidi na zaidi.

Leo kidogo tutupe jicho kwenye hii sekta ya hisa… Si sekta ngeni sana ila kwa hapa nchini wananchi wengi hawajaigundua na kushiriki kikamilifu kama nchi jirani na Tanzania. Wenzetu Kenya wamejitahidi kwenye ushiriki wa soko lao la Hisa la Nairobi (Nairobi Stock Exchange). Na kwa Afrika Mashariki, hili Soko la Hisa la Nairobi ndilo soko kubwa kuliko yote.

Soko letu la hisa la Dar es Salaam (DSE) japo kila siku limekumbatia usemi ni soko geni nchini, lina zaidi ya miaka  15 tangu lianze kufanya biashara mwaka 1998 mwezi  wa Aprili. Kwa muda wote huu wa miaka 15 soko limekuwa halina ukuaji  wa  kuridhisha  wala kuvutia. Mpaka leo 2013 kampuni zilizojisajili ni 17 tu, (Soma hapa zaidi http://www.dse.co.tz/main/index.php?page=5)  Idadi ya wananci wanaoshiriki kuuza na kununua hisa bado ni ndogo sana na uelewa wa jamii juu ya hili soko ni mdogo sana!

Pamoja na changamoto zake, hili soko lina faida kubwa kwa wale walioligundua na wanaoendelea kulitumia. Kuna mjasiriamali mmoja, yeye alinunua hisa za Twiga mwishoni mwa miaka ya 90 au mwanzoni mwa miaka ya 2000 zikiwa zinauzwa kati ya 200-300 kwa kipande. Leo hii kipande hicho hicho cha Twiga Cement kinauzwa kati ya 2500-2006 kiasi cha miaka 13 tu mbele.

Mdau huyu wa soko hilo anakiri kama angejua ukuaji ni wa kiasi hiki basi angenunua zaidi ya hizo alizonunuaga. Na ameendelea kuongeza vipande vyake kila awezapo. Anadai yeye hupenda kuwekeza kwenye hisa sababu hakuna usumbufu wa uendeshaji . Ukishanunua hisa unakaa na kungoja zipande ama zishuke ili na wewe uuze za kwako. Anakiri kuwa soko hili limemnufaisha sana na anawashauri wengine wajiunge nalo wapate kunufaika pia.

Wengi wetu wenye mitaji midogo midogo tunaweza kunufaika kwa kujiunga na hili soko la hisa la Dar es Salaam na kununua vipande kwa pesa tuliyonayo. Vipande vingi vimeonesha kupanda thamani yake ikiwemo hisa za makampuni ya bia (TBL na SBL), Saruji (Twiga  na Simba ) na Bank kama NMB. Kama mwekezaji mzalendo, ukijitosa ukanunua hisa zako za 2,000,000 leo, baada ya miaka 4 unaweza kuziuza hata kwa faida kubwa tu bila kuteseka na usumbufu wa uendeshaji kama zilivyo biashara nyingine.

Upande wa pili soko hili la hisa pia lina magumu yake kama kupotea kwa mtaji wako kutokana na kushuka kwa thamani ya vipande. Hili kwa mfano, limewaathiri wawekezaji walionunua hisa za CRDB na TOL ambazo zimekuwa zikikumbwa na kushuka kwa thamani mara kwa mara. Muhimu ni kuwa makini tu kwa kuchagua vyema ni hisa zipi ununue na kampuni ipi uwekeze.

Soko letu limekuwa likiwanufaisha zaidi wageni na wananchi wa nchi jirani ambao hulitumia kikamilifu kujinufaisha na wazalendo wengi kutoelewa nini kinachoendelea. Kwa wale waliokwisha jitosa, huwezi amaini jinsi wanavonufaika na kuwekeza zaidi na zaidi.

Huu ni wito wangu kwenu wazalendo wenzangu, mkajiunge na soko la hisa la Dar es Salaam na kufaidi matunda yake!

Elimu yetu Tanzania: Suala la kujifunza na changamoto za utandawazi

$
0
0

Poleni watanzania wenzangu kwa habari ya kusikitisha ya wahitimu wa Kidato cha Nne 2012 kuwa na ufaulu wa kusikitisha (zaidi ya 90% wamefeli kwa kupata div 4 au ziro). Kwa mzalendo yeyote lazima atajihoji ni wapi tunaelekea kama Taifa!? Kuna sehemu tumekosea, fuatana nami katika uchambuzi huu na nayakaribisha maoni yako…

Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa hali si shwari katika mfumo rasmi wa kupata elimu hasa kwenye suala muhimu la ubora. Ingawa nafasi za kusoma katika shule zetu za msingi, sekondari na vyuoni zimeongezeka jambo ambalo limetoa wigo mpana wa kuongezeka kwa uandikishwaji wa vijana wengi zaidi, lakini bado utata upo katika ubora wa elimu inayotolewa. Hii ni kwa elimu itolewayo na taasisi za umma na zile za binafsi. Ndiyo, hata katika taasisi za elimu za binafsi ambazo hivi karibuni zimekuwa zikipapatikiwa sana hususan na baadhi ya watanzania wenye uwezo bado viwango vya ufaulu na ubora wake ni duni!

Tafiti iliyoendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la UWEZO mnamo mwaka 2012 ilionyesha kuna tofauti ndogo sana ya ufaulu kati ya shule binafsi za Tanzania na zile za umma za nchini Kenya, ikiwa kiwango cha ufaulu wa asilimia 71 na 75! Hii inamaanisha, shule binafsi za nchini Tanzania zinautofauti ndogo sana kwa kiwango cha ufaulu (na ubora) kulinganisha na zile shule za umma kwa nchini Kenya licha ya kuwa kwa upande wa Tanzania, wazazi na walezi wanawajibika kulipa gharama kubwa sana wakati nchini Kenya katika shule za umma gharama ni nafuu. Hivyo kumbe inawezekana kabisa kuwa na shule za umma za gharama nafuu zenye elimu bora.

Kazi kubwa bado inatakiwa kufanyika ili watoto walio kwenye shule na taasisi mbalimbali za elimu nchini wajifunze na kuelimika kweli. Katika hili, serikali inapaswa kulipa suala la ubora wa elimu umuhimu mkubwa. Ukiacha hiyo ngazi ya kielimu, kuna elimu inayotolewa na vyuo vya ufundi kama VETA ambayo nayo inabidi iwekewe mkazo na isionekane ni elimu ya  wanaoshindwa kuingia kidato cha kwanza au kuendelea na kidato cha tano.

Pia na kuna elimu inayotolewa na vyuo vyetu vya elimu ya juu na vyuo vingine ambayo vinaanzishwa siku hizi kwa kasi na wingi ikiwa ni jitihada njema za kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya juu lakini  tunahitaji usimamizi wa hali ya juu katika ubora.

Kimsingi elimu ninayoieelezea ni iliyo katika mfumo rasmi na inategemea mitaala. Kufanya vizuri katika hatua moja kunakuwezesha kwenda kwenye hatua nyingine angalau kuna viwango na vigezo vimewekwa ili kufuzu. Licha ya matatizo yaliyopo kwenye mfumo rasmi wa elimu yetu nchini ambapo tunaweza kutupia mzigo wa lawama serikali na taasisi zinazotoa au kusimamia utoaji wa elimu hiyo lakini je tumeshajihoji na kujitathmini kuhusu tabia ya kusoma na kujielimisha sisi wenyewe? Kupeana msukumo katika kuelimika au elimu tunayoipata kuhakikisha inatukomboa?

Kwenye mazingira haya ya utandawazi  na kama pia tumekubali kuwa sekta binafsi na soko huria ndo itakayosukuma maendeleo ya nchi, hatuna budi kubadilika watanzania na hasa vijana kujielimisha wenyewe kwenye mambo mbalimbali iwe kwenye teknolojia, siasa (watu wengi hufikiri siasa ni ya wanasiasa lakini wakumbuke wote tunaathirika na maamuzi ya kisiasa. Rais wa zamani wa Ufaransa Charles de Gaulle alisema; “I have come to the conclusion that politics are too serious  matter to be left to the politicians” Tafsiri yangu ikiwa; nimefikia hitimisho kwamba siasa ni jambo la msingi mno kuachiwa wanasiasa ) pia kwenye uchumi, michezo na nyanja mbalimbali.

Kwa mfumo wa uchumi wa dunia ya sasa milango imefunguka kiasi kwamba muingiliano baina ya watu wa mataifa umekuwa mkubwa na maisha ya mwanadamu yamekuwa ya ushindani mkubwa wa rasilimali ambazo hata kama zipo kwenye mipaka yetu lakini watu wengine duniani wanazitamani. Ili tuwe  washindani duniani hatuna budi kuuelewa ulimwengu wa sasa na mifumo yake nje ndani hatuna jinsi.

Ni muhimu kuwa na serikali na taasisi zenye nguvu sio tu nguvu ya serikali dhidi ya raia wake kwa maana ya kubinya haki za raia wake, au kutawanya maandamo, bali inayoongozwa na watu wanaoelewa mazingira ya sasa ya dunia hii ya ushindani ya jinsi kama taifa linavyoweza kushiriki na kupata faida kwenye utandawazi. Tuna jukumu la kuhakikisha tunakuwa na serikali ya aina hiyo. Serikali kama hiyo inaweza kupatikana tu kutokana na aina ya jamii tuliyo nayo, ndiyo maana ni muhimu sana kuwa na jamii iliyopata elimu bora katika mazingira rasmi na kwa jitihada binafsi za kujielimisha. Tukumbuke wengi tunaowalalamikia kwa utendaji mbovu kwenye serikali zetu na sekta binafsi wanatoka miongoni mwetu!

Udadisi binafsi wa kujifunza ni mdogo sana miongozi mwa watanzania, achilia mbali ongezeko la fursa za  kusoma kutoendana na kuongezeka kwa ubora watanzania walioelimika inashabiri ukweli kuwa wengi wa watanzania wanaopitia mifumo ya kielimu hukosa muda wa kujifunza kwa mfano wa kujisomea wenyewe hasa baada ya kutoka kwenye mfumo rasmi wa elimu. Kwa hiyo kuna mchanganyiko wa hatari yaani; utolewaji wa elimu isiyo na ubora  sambamba na uvivu wa kujifunza miongoni mwa wanajamii.

Waajiri wengi hususan kwenye zama hizi za ushindani wamekuwa wanalalamikia viwango duni vya watu wanaozalishwa kwenye shule na vyuo vyetu. Kwenye ripoti ya chama cha waajiri Tanzania (Association of Tanzania Employers) na wadau wengine kama shirika la kazi duniani (ILO) inayoitwa Business Agenda-Tanzania  ya mwaka 2011 inasema; kuna upungufu mkubwa wa ujuzi kwenye sekta binafsi kwenye ngazi zote .Ufanisi umekuwa mdogo kulinganisha na jirani zetu kama  Kenya na nchi nyingine zinazoendelea kama China na India. Ripoti hiyo pia inabainisha kwamba ili tutoke hapo tulipokwama ni lazima tuongeze ubora kwenye elimu inayotolewa kwenye shule za msingi, sekondari, vyuo vya ufundi na elimu ya juu.

Shida kubwa ya elimu yetu rasmi ni kwamba haitufundishi kujifunza. Hata waliopo kwenye vyuo vikuu hawana ari ya kujifunza zaidi ya kusoma kwa ajili ya kufaulu mitihani na majaribio. Mtu anaweza kumaliza elimu ya juu bila kugusa kitabu! Ni jambo la hatari sana hili. Tumepunguza na kuhalalisha suala zito la kujielimisha mpaka kwenye kupata vyeti tu. Huo ndio umekuwa msukumo wa wengi, kupata vyeti kumekuwa  motisha mashuleni na vyuoni kunakowafanya watu wakariri chochote.

Tumefikia uthubutu hata wa kununua au kulipa fedha kuandikiwa tasnifu (dissertation) alimradi tuweze kupata shahada badala ya kufanya utafiti kwa tija ya kuibadili, kuifahamisha na kuikomboa jamii yetu!

Uchumi wa kisasa unahitaji watu walioelimika vyema na walio tayari kuendelea kujielimisha hata baada ya kutoka shuleni na vyuoni.  Mwandishi Ruchir Sharma kwenye kitabu chake kinachoitwa;  Breakout Nations in pursuit of the next economic miracles  anatoa mfano wa kampuni ya vifaa vya kompyuta ya intel mwaka 2010 ilivyokwama.Kampuni hiyo ilitaka kuwekeza kwa kufungua kiwanda cha kutengeneza vifaa vya kompyuta nchini Vietnam kwa kiasi cha dola za marekani bilioni moja, na walihitaji wafanyakazi 4,000 wenye ujuzi wa kawaida wa ufundi  na wenye kujua kiingereza kidogo lakini walipowasaili watu 1,200 wa kwanza walipata watu wenye sifa hizo wanne tu! Mpaka sasa wameshindwa kufikia lengo la kupata wafanyakazi wenye ujuzi wanaoutaka kwa idadi hiyo ya 4,000, na labda mpaka mwaka 2016 ndio watafikia hiyo idadi na hiyo ni baada ya kuanza kuwafunza watu wao wenyewe. Hapa kuna funzo muhimu sana hasa nyakati hizi ambapo neema za rasilimali kama gesi, mafuta na madini zinaendelea kugunduliwa nchini mwetu.

Tuwekeze vizuri kwenye elimu rasmi. Watu wafundishwe kujifunza. Elimu iwakomboe, tujue kujifunza ni zoezi la kudumu. Lakini kama tunataka tu kukimbia ovyo ovyo na tusijue tuendapo basi njia yoyote itatufaa.

KITAMBI: Chanzo chake na jinsi ya kukiondoa

$
0
0

Kitambi (kilibatumbo) ni tumbo kubwa ambalo linachomoza kwa mbele na wakati mwingi kuning'inia isivyo kawaida. Ni ugonjwa kama magonjwa mengineyo na huweza kuwakumba watoto, vijana, watu wazima na hata wazee wa jinsia zote!

Kwa baadhi ya watu, hukichukulia kitambi kama ishara ya ufanisi au mafanikio kwa mhusika katika nyanda nyingi za kijamii. Ni imani ambayo kwa namna moja ama nyingine inachekesha kwakuwa kilibetumbo ni ugonjwa kama magonjwa mengine.

Mwili wa binadamu una seli bilioni 50-200 za mafuta zilizogawanyika kwenye mwili wa binadamu. Kwa wanawake zipo sana maeneo ya matiti, nyonga, kiunoni na kwenye makalio. Kwa wanaume seli zipo sana kwenye kifua, tumboni na kwenye makalio.

Mafuta ya tumbo yanayofanya kitambi hukusanywa kwa njia kuu mbili, ya kwanza ni mafuta kutoka kwenye tishu zilizo chini ya ngozi na ya pili ni kutoka kwenye ogani za ndani kama moyo, kongosho n.k

SABABU ZA KUPATA KITAMBI:

Sababu kubwa ya kitambi ni kukosekana ulingano wa nguvu(kalori), mtu kula vyakula vinavyotia nguvu sana kuliko jinsi anavyoweza kutumia na kutoa kama taka mwili.

Vyakula vinavyochangia uongezekaji wa kilibetumbo ni pamoja na nyama (iwe ni ya kuchemsha, kukaanga au kuchoma), mafuta ya kupikia, (hasa yale yatokanayo na bidhaa za wanyama, kama siagi, na jibini), viazi ya kukaanga (chips), pizza, vyakula vyenye wanga mwingi kama ugali wa mahindi, mihogo, wali, mikate myeupe na pia viazi vya mviringo. Ndizi pia huchangia!

Sababu nyingine ni kuwa na chembe za urithi za unene kutoka kwa wazazi, pia kuna sababu za kimazingira. Ila pia kuna sababu nyingine zisizojulikana.

JINSI YA KUJUA KAMA UNA KITAMBI:

Kitambi kinaweza kuonekana kwa kirahisi kwa macho. Ila kujua ni kwa kiwango gani kitambi chako kipo inabidi kufanya vipimo vya kiuno(waist) na nyonga (hips). Mzingo wa kiuno ukiwa >102 cm au 40 in kwa wanaume na >88 cm au 35 in kwa wanawake, na uwiano wa kiuno na hips(Waist-Hip Ratio) ikiwa >0.9 kwa wanaume na >0.85 kwa wanawake.

BMI ya 30 au zaidi inaashiria 'Obese' uzito kuzidi kiasi. Kuwa na mzingo uliozidi kawaida ni kiashiria hatari cha matatizo ya kimetaboliki, kuliko hata cha BMI.

Kipimo kingine cha kitambi ambacho kimeonyesha uwezo zaidi kuliko BMI katika kutabiri uwezekano mkubwa wa magonjwa ya moyo ni Index Of Central Obesity(Waist-To-Height Ratio-WHtR) ambapo uwiano ukiwa sawa na 0.5 au zaidi, hii ikimaanisha mzingo wa kiuno angalau ni nusu ya kimo cha mtu.

Kipimo kingine ni Body Volume Index, kinachopima kitambi kwa kupima umbo la mtu na mgawanyo wa uzito wake.

NJIA ZA KUONDOA KITAMBI:

  • Mlo mzuri kiafya ndio ufunguo wa kupunguza uzito na kutoa kitambi. Kuacha kula vyakula vinavyotia nguvu sana, vyenye mafuta na sukari nyingi ndio msingi wa kuondoa kitambi. Hii husaidia mwili kutumia mafuta yaliyo mwilini kutengeneza nguvu hivyo kupunguza mafuta na kuondoa kitambi. Aidha, punguza matumizi ya vinywaji vyenye sukari kwa wingi na tumia samaki badala ya nyama.
  • Kufanya mazoezi ya mwili kila siku kwa dakika 30-60 walau siku 3 ndani ya juma (week) moja (Mfano kuendesha baiskeli na kukimbia).
  • Dawa ni muhimu tu kama una matatizo mengine kama kisukari, mfano dawa fulani za kisukari zinaweza kukusaidia kupunguza mafuta yanayozunguka ogani muhimu kama ini na kongosho.
  • Kufanya upasuaji mkubwa ili kupunguza mafuta, hii hufanyika kwenye nchi zenye teknolojia kubwa na hii hushauriwa endapo mafuta yaliyomwilini yamesababishwa na magonjwa yameshindwa kupungua kwa njia ya rahisi ya kawaida.

Imedhihirika pia kudhibiti 'Stress' inaweza kusaidia kwenye kupambana na kitambi.

Digiti sawa, zi wapi chaneli tano muhimu?

$
0
0

Wahenga walinena; “Ahadi ni deni”. Katika mchakato wa kuingia kwenye mfumo wa kurusha matangazo kwa njia ya digiti toka mfumo wa analojia, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano iliwaahidi watanzania; wataendelea kupata fursa ya kutizama chaneli za ndani. Iliahidi ving’amuzi vingalirusha bure chaneli tano muhimu za ndani zisizo za kulipia ambazo ni; ITV, Channel Ten, TBC1, EATV na StarTv.

Miezi miwili mpaka sasa toka kuingia katika mfumo wa digiti ambapo siyo ving’amuzi vyote vinarusha chaneli tano muhimu kama ahadi na uthibitisho uliotolewa.

digital-tanzania

Ifahamike kuwa, hakukuwa na muongozo wa king’amuzi gani mwananchi anapaswa anunue ambao ulitolewa hapo awali ili kumhakikishia mlaji kupata huduma bora na hasa kupata kuona chaneli muhimu za ndani. Ila tu kila mwananchi wenye kuhitaji wa kupata matangazo ya luninga alihamasishwa kununua king’amuzi ili aweze kupokea matangazo yaliyoanza kurushwa kwa mfumo wa digiti tofauti na mfumo wa analojia ambapo haikuwalazimu kuwa na king’amuzi.

Ni kweli, makampuni binafsi ndiyo yamekuwa vinara kwa muda mrefu hata kabla ya kuingia katika mfumo wa digiti yamekuwa yakiendesha biashara ya kurusha matangazo kwa njia hiyo kwa kutumia ving’amuzi. Asilimia kubwa ni makampuni ya kigeni.

Hata nchi ilipoingia katika mfumo wa digiti, na hivyo hitaji la kutumia ving’amuzi kukua bado tegemezi la huduma ya kupokea matangazo kutumia ving’amuzi imekuwa chini ya makampuni binafsi.

Ni kampuni moja tu ambayo serikali ina hisa. Kampuni ya Star Times International Communication yenye king’amuzi chao cha StarTimes ambapo serikali kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) lina hisa asilimia 35 huku wawekezaji toka China wakiwa na asilimia 65.

Suala la mkataba baina ya kampuni ya Star International Communication na Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) na hasa afya na ustawi wa Shirika la TBC ni suala pana ambalo linastahili makala ya kujitegemea tofauti na hii.

Tukiachilia mbali ubora duni wa baadhi ya ving’amuzi katika kurusha matangazo yake ambao wateja wengi wameshaonyesha kutorishishwa, suala la kupata matangazo toka chaneli za ndani limekuwa ndoto kwa ving’amuzi vingi nchini.

Ni makampuni yasiyozidi matatu yenye kutoa huduma kupitia ving’amuzi ambao angalau kidogo wamemudu kutoa huduma ya chaneli za ndani hususan zile tano muhimu.

Licha ya kumudu kurusha matangazo ya chaneli muhimu tano za ndani makampuni hayo pia yameungana na makampuni mengine kuenenda kinyume na ahadi ya mamlaka ya TCRA kuwa huduma ya chaneli tano muhimu zinapaswa kutolewa bure hivyo hata kama mteja hatomudu kulipia gharama ya kupokea matangazo kwa mwezi husika aweze kuendelea kutizama chaneli tano muhimu. Hili nalo linakiukwa.

Katika mazingira hayo, wananchi ambao wamekuwa wakipambana kuhakikisha wanapata huduma ya taarifa za ndani wamekuwa wakilazimika kununua na kuvigharamia ving’amuzi zaidi kimoja. Hili halikubaliki!

Suluhu kama hii ni suluhu ya mtu mmoja mmoja, si suluhu ya kijumuiya kwa manufaa ya wengi. Si kila mwananchi ambaye anaweza kumudu kununua na kugharamia ving’amuzi zaidi ya kimoja. Hivyo ni muhimu sana kuhakikisha kila raia analindwa.

Hatupaswi kuruhusu taifa kuendelea kuacha raia watafute suluhu ya mtu mmoja mmoja kwani ndiyo inayoligawa na kuligharimu Taifa mpaka sasa.

 Tumeshuhudia pale ambapo baadhi ya wananchi walianza kuwa na mashaka na ubora wa elimu inayotolewa na shule za umma wamekuwa wakiwapeleka vijana wao katika shule binafsi huku shule za umma zikizidi kudidimia katika uduni na hali mbaya ya kimazingira ya kielimu. Zao la hali hiyo ni pamoja na ufaulu duni hasa katika shule nyingi za umma!

Suluhu binafsi inaweza kuonekana pia katika nyanja nyingine nyingi kama vile mazingira mabaya ya huduma za usafiri hususan katika miji na kila mwananchi mwenye uwezo kukimbilia kutatua kwa kuwa na usafiri binafsi huku ule usafiri wa umma kuzidi kuwa katika mazingira duni mathalani kubeba abiria wengi sana kuliko inavyopaswa..

Mifano katika sekta ipo mingi sana, iwe afya, nishati ya umeme, maji nk kote kuna uduni na mfumo umeacha wananchi watafute suluhu yao binafsi na si suluhu ya kimfumo mzima.

Miongoni mwa majukumu ya mamlaka mbalimbali kama ilivyo kwa TCRA ni kusimamia na kuratibu shughuli nzima za sekta husika. Hivyo, kwa TCRA kusimamia suala la kurusha na kupokea matangazo kutoka kwa kampuni kwenda kwa wananchi ni miongoni mwao.

Ni kama vile mamlaka ya EWURA inavyosimamia na kuratibu masuala mazima ya nishati na maji. Hivyo kuweza kusimamia mathalani bei za nishati ya mafuta na kuwasimamia ipasavyo wafanyabiashara.

Wananchi wengi kwa nyakati tofauti wamekuwa wakihoji, iwapi haki yao ya kupata taarifa inazingatiwa? Ni kwanini mamlaka na taasisi za kiserikali husika zinashindwa kuhakikisha kila mtanzania anamudu kuona hasa chaneli tano muhimu kama vile ahadi ilivyotolewa?.

Licha ya mchakato mzima wa kuingia katika mfumo wa digiti kuwanyima haki wananchi kupata taarifa lakini pia kutokuweza kusimamia wafanyabiashara na makampuni husika ambayo yanatoa huduma za kurusha matangazo kwa wananchi imeshtusha wengi.

Ikumbukwe, suala la kupata habari na kusambaza habari ni haki ya kila raia kikatiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mujibu wa ibara ya 18 (b); “kila mtu anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila kujali mipaka ya nchi” lakini vile vile kipengele 18 (d) “kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii”.

Lakini jukumu hili pana la kuhakikisha haki kwa wananchi linawakumba pia wadau wengine mathalani baraza la walaji la sekta husika. Mabaraza ya walaji yanapaswa kuhakikisha walaji (wananchi) wanapata huduma stahiki na kwa ubora.

Mpaka sasa hakuna mikutano ya mara kwa mara kusikiliza wananchi “public hearings” ambayo ni moja ya njia za ufanyaji kazi wa mabaraza haya kupata mrejesho wa wananchi katika upatikanajihuduma.

Katika kipindi hiki cha nguvu ya soko huria ambapo mikono ya serikali inaondoka katika uchumi wa soko suluhu na matumaini ya wananchi daima imewekwa katika mabaraza. Mabaraza yanapaswa kuwa watetezi wakuu wa walaji. Ndiyo mantiki kuu hasa ya wito wa aliyekuwa rais wa awamu ya tatu wa Tanzania yaani; “tunaondoa mikono ya serikali kwenye uchumi wa soko lakini hatuondoi macho ya serikali”.

Na ndiyo hata hofu ya baadhi ya wananchi juu hasa ya hatari ya mazingira ambapo mabaraza ya walaji yakiwa yana hisiwa kuenenda kama vile yapo katika ndoa na watoa huduma na wadhibiti, daima walaji ndiyo wanaoumia kutokana na hali hiyo.

Katika hali ya mabadiliko ya kasi ya sayansi na teknolojia hususan upashanaji wa habari kwa njia ya TEHAMA, bado pia mabaraza hayajachukua fursa hiyo kukusanya maoni na mrejesho wa kutosha wa wananchi juu ya maoni yao katika utolewaji wa huduma mathalani hii ya digiti kwa kupitia ving’amuzi. Wananchi wengi wamekuwa wakionyesha kutokuridhishwa kwao huku madai hayo yakielea hewani bila hatua madhubuti kuonekana zinachukuliwa.

Katika nchi nyingi zilizopiga hatua hasa katika kusimamia na kupigania haki za raia wao, mabaraza na watendaji wakuu wa mabaraza mathalani wenyeviti wananguvu sana katika jamii zaidi au sawa hata na wanasiasa.

Lazima wananchi waamke kudai haki yao ya msingi ya kupata taarifa, kwani kutokupata taarifa kunarudisha nyuma kwa kiasi kikubwa juhudi zote za kimaendeleo. Na ndiyo maana hata kuna usemi wa; “information is power”! (yaani; taarifa ni nguvu).

Na ndiyo maana hata katika mapinduzi ya serikali za nchi, vituo vya habari ni miongoni mwa sehemu muhimu sana ambazo wahusika wa mapinduzi huvilenga!

Kwa hivyo basi, endapo kwa makusudi au kwa bahati mbaya na kuendelea kuachwa kwa hali ya kutokuwa na fursa kwa wananchi wengi kutokupata taarifa kwa wananchi ni kudhibiti nguvu ya wananchi. Ni  njia na mbinu moja wapo ya kuwadhibiti.

Tumefikia kuwa na Taifa ambalo wananchi wake wamegawanyika. Wapo wananchi ambao hawamudu kabisa kupata habari kutokana na kutokumudu gharama za manunuzi na uendeshaji wa ving’amuzi. Lakini pia wapo wananchi ambao kutokana na udhaifu wa kimfumo wakosa kuona chaneli za ndani muhimu si kwamba hawana king’amuzi au wameshindwa kuvilipia bali huduma ya chaneli tano muhimu hazimo katika ving’amuzi ambavyo wanatumia. Wamekuwa watanzania ambao wanalazimika kutizama chaneli za nje zenye habari za mataifa mengine ndani ya nchi yao kuliko kutizama chaneli za ndani ili kupata habari za ndani ya nchi.

Ni wakati sasa wa kuchukua hatua. Ni wakati sasa kwa kila raia mmoja mmoja na kwa kuungana kuhakikisha tunawasilisha kutoridhika kwetu na namna ya mifumo ya upashanaji habari inaendeshwa nchini katika mamlaka husika kama vile Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), katika baraza la walaji la sayansi na teknolojia na katika wizara husika. Ni jukumu na wajibu wa kila raia kuhakikisha anaiwajibisha serikali pale haienendi katika misingi ya haki.

Kwa hatua na matendo yetu ndipo tutamudu kuonyesha utofauti kati ya “watawaliwa” (subjects) na “raia” (citizens) katika Taifa letu. Hayati Bob Marley alipata kuimba; “how long shall we stand a side and look…while injustice prevails” (Ni mpaka lini tunaendelea kusimama kando na kutizama….vitendo vya uvunjifu wa haki vikimea).

Wakati ni sasa!

NGONO: Wanawake na Wanaume tunapoamua ‘kujiachia’ na Madhara yake…

$
0
0

Msomaji, nimeona vema nishirikiane nawe katika hii hoja ya kujiachia kwa miili yetu katika kufanya mapenzi na wapenzi wetu. Hapa ninaposema kujiachia sina maana kujiachia wakati wa faragha kufurahia tendo… Bali nazungumzia kujiachia kwa bahati mbaya ama makusudi na kutojali ama kuzingatia ni idadi ngapi ya watu unashirikiana nao iwe kwa siku, juma (wiki), mwezi ama hata mwaka.

Suala lililopo hapa (hasa kwa akina mama/dada) wengi hujiweka katika kundi la kutokujiachia ovyo. Kwako msomaji naomba tulia na jitafakari ukiwa mkweli kwa nafsi yako kama upo kundi hili la kujiachia.

Kujiachia kupo tofauti, kuna kujiachia unakuwa na mpenzi mmoja mmoja lakini hadumu zaidi ya miezi mitatu hivyo kukufanya uwe umelala na walau watu 4-6 kwa mwaka (hivo kama ulianza huo mchezo kaika umri wa miaka 17 na upo miaka 25 ina maana umeshawahi lala na wanaume si chini ya 25).  Pia kuna kujiachia kwa kuchanganya wapenzi ama kutoka nje ya mahusiano ya mpenzi/mwenza wako. Huku kutoka kama ni kubadilisha kila siku huko nje ndiyo kujiachia kwenyewe na nafuu huwepo kwa yule ambaye ana-maintain mtu huyo anayetoka naye. Hata hivyo tuangalie sababu ambazo hutufanya tujiachie ni zipi…

Sababu za Wanawake na Wanaume Kujiachia

Kuwa na Mpenzi asiyemridhisha, inaweza tokea mtu ana mtu wake anampenda sana na wapo pamoja kama couple ila hatosheki kabisa wanapokuwa faraghani. Siku za mwanzo atajitahidi kuvumilia, ila inapotokea tayari starehe ya kutaka kufikishwa imemvaa, aweza jikuta akajiachia kwingine.

Kuwa na tamaa ya vitu hivyo kujiachia kwa kuhongwa kama namna ya kupata alicholenga. Hii ilikuwa sana kwa wanawake, ila tokana na kushuka kwa maadili kasi inaongezeka na kwa vijana wa kiume pia. Anaweza kuwa na mpenzi wake ama wapenzi wengi kwa ajili ya kuwa na machimbo tofauti ya kupata pesa ya kujikimu tamaa zake za vitu. Kwa vijana mara nyingi hutolewa na wamama maarufu kama Jimama.

Kuwa desperate sana na kutoweza ishi bila Mpenzi, kila anapoachika mara kishampata mwingine. Kuna kundi la watu hawawezi kabisa kuweka nafasi (gap) kubwa kati ya mpenzi wake ambaye kaachana naye na mpenzi mpya. Hii husababisha mhusika kujikuta yupo katika mahusiano na mtu ambaye hamfai na hivyo kuachika na kutafuta tena. Mwisho wa siku ndani ya mwaka wapenzi siyo chini ya 6.

Kuwa addicted kwa ngono (Hii ni wachache kwa wanawake na wengi wa wanaume) Huyu mtu anataka kufanya ngono mara kwa mara. Inapotokea mtu mpenzi wake hayupo atajitahidi kwa kila namna atafute mbadala ili kujiridhisha.

Kuwa tu na hulka ya Umalaya/Uhuni. Anakuwa kishazoea kuwa na wapenzi wengi… Hawezi kuwa na mpenzi mmoja, hawezi tulia katika mahusiano, kila siku kutafuta sababu za kuwa na mtu zaidi ya mmoja. Na huona kuwa hiyo ni part ya maisha yake na kuwa afanyalo ni sawa.

Ushawishi wa makundi… Inaweza kuwa kama mzaha na wengine wakadhani kuwa mtu mzima huwa na akili yake independent katika maamuzi. Kwa mtazamo wangu, makundi yanachangia sana kwa baadhi ya watu kujenga tabia ya kujiachia na kuona ni sawa hali awali asingeweza thubutu.

Ngono kuwa ndicho chanzo cha kipato cha kila siku, hii ni kwa wale ambao ngono hutumika siyo tu kwa starehe. Ngono huwa ni chanzo cha kipato… Makundi yametofautiana, kuna wale ambao ni wa hali ya juu na huchaji kwa bei za juu na pia kuna wale wa viwango vya chini na viwango vya chini pia wote tegemeana na maeneo wanayopatikana.

Kutojitambua na hivyo kuwa na huruma sana ya kumfanya kutoweza kabisa kukataa akiombwa tunda lake. Hii ni kwa wanawake ambao hawawezi kabisa kusema ‘NO’. Hata kama hamtaki huyo mtu yeye humuonea huruma na kuona ni kheri tu akamalizane naye akamsaidie haja zake.

Kuwa na kilevi katika maungo ya watu wawavutiao. Mfano kuna mwanaume akiona mwanamke mwenye makalio makubwa anachanganyikiwa kabisa na hujitahidi kwa kila namna ampate huyo mwanamke. Kama vile baadhi ya wanawake wanavyoweza changanyikiwa kabisa na kifua, sura ama hata sauti ya mwanaume to the extent atajitahidi kwa kila namna kuweka mazingira ya huyo mwanaume amtongoze ili atimize kiu yake.

Kwa wanaume zinaongezeka;

Kuongeza kujiamini (confidence) na Ufahari kuwa yeye ni mwanaume kamili na lijali – Cha kusikitisha hapa ni kuwa siyo wanaume wote ambao wanalala ovyo wana uwezo wa 6/6.  Ila sababu mara nyingi wanawake tumejenga utamaduni wa kujificha hisia za kweli wakati wa tendo, wengi sababu ni wa kupita tu kwa huyu mwanaume humezea tu rohoni kwa uwezo wake mbovu katika uwanja huo wa faragha… Hasa kama ana pesa ndiyo kabisa!

Madhara ya Kujiachia kwa Wanawake na Wanaume pia…

Madhara kwa Ujumla wake – Wanawake madhara ni makubwa zaidi ya wanaume… It is not fair, ila ndiyo ukweli wenyewe! Kwa mwanamke kubadilisha wapenzi mara kwa mara, kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja na ikajulikana wazi, kutoka nje ya ndoa kwa kiasi kikubwa sana humbomolea heshima mbele ya jamii na cha ajabu zaidi kwa wanaume wenyewe! Kitendo kama vile mwanamke kuwa katika kundi la wanaume ambao zaidi ya mmoja wameshawahi lala naye na inatambulika ni wazi kuwa maongezi kila ugeuzapo mgongo huwa siyo mazuri juu yako. 

Maisha yamebadilika sana na tokana pengine na mazingira na kukosekana na wanaume ambao wana sifa ya kuwa wanaume inaweza changia kwa kiasi kikubwa mahusiano kutofanikiwa. Kimsingi inatakiwa umakini, hekima, subira ya kuweza kupata mtu ambaye anakufaa kuwa mtu wako kwa muda mrefu. Ni rahisi kusema na ngumu kutenda lakini inawezekana.

Bahati mbaya saana ni kuwa kuna baadhi ya wadada huona kama mzaha na kuona kuwa kuna viwango (standards) vipo sawa katika kumtazama mwanaume ambaye anabadilisha girlfriends mara kwa mara kama vile yeye ambavyo hubadilisha boyfriends mara kwa mara. Lakini with time hukua na kupevuka akili na kutambua kuwa hailipi…. Ama huamua kujilipua hadi utu uzima kwa kujua kuwa kama damage ishafanyika.

Pamoja na kuwa kunaweza kuwa mwanaume na mwanamke wenye sifa sawa kabisa katika kujiachia katika ngono; reputation ya hao watu katika jamii ni mbili tofauti. Na hata mwanaume akilaumiwa kama amekithiri atalaumiwa siyo kwa kuwa na wanawake wengi, bali kwa kutembea ovyo ovyo hata na wale ambao wanamchafulia tu jina na sifa zake.

Madhara Mengineyo:-

  1. Inaweza leta kutokujiamini kwa mhusika hasa kwa wanawake… Kila mara kujichunguza kasoro alizo nazo na kujiona kana kwamba ana nuksi ya kuachwa mara kwa mara. Na kama ni mzuri hili ndiyo humchanganya kabisa na kuweza kujikuta yupo kwa mganga na hali mchawi ni yeye mwenyewe.
  2. Inaweza leta tafrani kwa wale ambao wamechanganywa watakapo tambua kuwa wamechanganywa. Kuna wengine hupata hasa cha moto, na wengine huponea chupu chupu kudhurika tokana na tabia hizo.
  3. Kuvunjika kwa ndoa. Hii ni mara nyingi mwanaume anapomfumaniya mkewe. Kwa wanawake wengi husamehe makosa ya kusaliti kwa waume/wapenzi zao kwa sababu zozote zile ambazo hubeba wao. Ni mara chache wake huacha waume zao sababu ya wao kuwa na wapenzi nje.
  4. Kuchuja kwa uzuri hasa kwa wanawake… Wadada/mama wengi hupungua uzuri wao hasa nuru katika sura zao.
  5. Kushuka kwa maadili. Wakubwa katika jamii wamekuwa wakichukulia suala la mahusiano kwa wepesi na saa nyingine kutozingatia mazingira na hadhira na kufanya baadhi ya mambo mbele za watoto wadogo wanaokuwa na kuiga tabia za kujihusisha na mapenzi.
  6. Kushuka kwa heshima ya mhusika kwa jamii iliyo mzunguka tokana na matendo yake hayo.
  7. Magonjwa hasa ya zinaa na kuzidi kuongezeka kwa kasi kwa HIV/AIDS.

Usalama wa wanahabari na rushwa: Mjadala uliokwama

$
0
0

Leo tarehe 27 Machi 2013 ilikuwa siku nyingine ambapo wanahabari wameshindwa kufikia muafaka juu ya suala la usalama wao.

Mjadala huu uliandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) lengo likiwa ni kutafuta mbinu ya kujilinda hususani baada ya kushambuliwa kwa mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Absalom Kibanda. Mada ilikuwa “Usalama wa Waandishi wa Habari Tanzania”

Kwa sura iliyojitokeza leo ni kwamba wanahabari wanapenda kuwakosoa watu wengine lakini hawapendi kujikosoa wao wenyewe wala kukosolewa.

Mjadala ulichochewa na mtoa mada Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Bi Valerie Msoka ambaye alianza kuchanganua adui wa mwanahabari ni nani hasa.

“Nimebahatika kufanya kazi na vyombo mbali mbali vya habari kama vile BBC na hata Umoja wa Mataifa kila niendako kama mwanahabari niliweza kumfahamu adui yangu ni nani, kwa hapa Tanzania ni vigumu kumfahamu adui yangu mimi kama mwanahabari” anasema.

Akifafanua zaidi kauli yake hiyo anasema katika nchi alizopata kuzitembelea wale waliokuwa ‘maadui wa watu’ au wa wananchi katika ujumla wao ndiyo pia walikuwa maadui wa wanahabari.

Anasema hali ilikuwa hivyo Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Uganda Kaskazini, Sudan ya Kusini, Iraq na hata Libya, lakini kwa Tanzania anasema inakuwa vigumu sana kujua namna ya kujikinga kutokana na aina ya mashambulizi yanayofanywa.

“Je adui yangu ni nani? FFU, Usalama wa Taifa, vyama vya siasa? Nauliza kwa sababu wala sijui ni chama gani kinatuma watu ili kuwashambulia wanahabari, hali hii inanitatiza sana,” anasema Msoka. 

Anakumbusha mauaji ya Daud Mwangosi, Issa Ngumba, na hata mashambulizi kwa wanahabari yaliyofanyika Mtwara hivi karibuni kwa kile kilichodaiwa kwamba wanaripoti kwamba mgogoro wa gesi umekwisha wakati bado upo.

Anauliza  je adui yangu ni mmiliki wa chombo cha habari? Mwisho anasema anachokiona ni woga na anawaasa waandishi watafute namna bora ya kuripoti inapotokea mwanahabari amedhuriwa kama ilivyokuwa kwa Mwangosi kwani tukio hilo liliripotiwa katika namna ya kuwaogofya na kuwavunja moyo wanataaluma wengine husuani wanawake.

Baada ya Msoka alikuja mualikwa mwingine Prof. Nicholls Boas, Mtanzania anayefundisha taaluma ya habari nchini Marekani ambaye alionekana kutema sumu ambayo ilileta mzozo kidogo ukumbini hapo New Africa Hotel.

Msomi huyo anasema kwamba vyombo huru (binafsi)  vya habari ndivyo vyenye uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko katika nchi yoyote. Anasema vyombo vinavyomilikiwa na serikali kama TBC na Daily News ni kwa ajili ya propaganda za serikali ambazo zinaweza zisiwe na manufaa kwa wananchi wote katika ujumla wao.

Zaidi ya hayo msomi huyo anasema kwamba katika nchi nyingi zilizokuwa katika mfumo wa chama kimoja kinachojiona kimo hatarini kung’olewa madarakani ni kawaida kutumia jeshi la polisi, maafisa wa usalama wa taifa na hata mahakama ili kubakia madarakani. Na vivyo kuwatisha na hata kuwaua wanahabari huwa ni mkakati wa kuzimisha sauti pinzani.

Mwanasheria mbobevu profesa wa sheria na Mwenyekiti wa Umajumui wa Kiafrika (Pan-Africanism) Issa Shivji anasema haitoshi kuzungumzia usalama wa waandishi wa habari wakati wanajamii wote wapo hatarini anakumbushia tukio la hivi karibuni ambapo askari polisi alimuua kwa risasi mwendesha boda boda na yeye (polisi) akauawawa kwa mawe.

Wakati mjadala ukiendelea ilionekana kuna kauli  iliwakera baadhi ya wahariri waliopata kufanya kazi Daily News na wale ambao bado wameajiriwa na kampuni anayochapisha gazeti hilo. Wa kwanza alikuwa mhariri mmoja mkongwe nchini aliyesema kwamba hakuna serikali yoyote duniani isiyokuwa na chombo cha habari ikiwamo Marekani na VOA, Uingereza na BBC.

Baadaye alisimama mhariri wa Daily News Bw. Deo Mushi akasema vyombo vya serikali ndivyo vinazingatia maadili zaidi kwa sababu waajiriwa wake wanalipwa mishahara na haki zingine stahiki.

Kinyume chake baadhi ya makampuni binafsi hufikisha hadi miezi mitatu kabla hayajawalipa waandishi mishahara yao hali ambayo husababisha wengine wakiuke maadili yao na kuanza kuchukua hongo hivyo kuidhalilisha taaluma hiyo adhimu.

Hoja hiyo ilimuibua Katibu Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), mhariri mkongwe Mzee  Henry Muhanika ambaye alisema mjadala ulikuwa umeandaliwa kwa ajili ya masuala ya usalama na wala siyo maadili wala maslahi ya wanahabari.

Mara Prof. Boas aliibuka na kusema maslahi ni sehemu ya usalama wa wanahabari. “mwandishi hawezi kuwa na usalama iwapo ana njaa, njaa tu yenyewe ni tishio la usalama wa wanahabari.

Akionekana kumuunga mkono profesa huyo alikuwa Lilian Timbuka kutoka magazeti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyesema kwamba baadhi ya magazeti ya kampuni binafsi yanaandika sana habari za kununuliwa (pr stories) hali inayoonyesha kwamba habari hizo hupikwa na wale wanaozilipia kwa wanahabari.

Lakini Prof akaibuka tena na kuvitetea vyombo binafsi kwa nguvu zote. Ndipo yule mhariri mkongwe aliyepata kuwa Daily News akaamuka na kusema prof. asiongee kama kibaraka wa nchi za magharibi na kwamba anajua tu nadharia lakini hajawahi kufanya kazi katika chumba cha habari hivyo hana haki ya kuyasema yale ayasemayo.

Kidogo amani ipotee hivyo ilibidi mhariri aondoke ili kulinda amani katika mdahalo huo. Mhariri Godfrey Lutego anasema adui namba moja wa wanahabari ni wanahabari wenyewe kwa kukosa maadili na kukubali kutumiwa na wanasiasa wenye tamaa ya madaraka wakiwamo mafisadi.

Lutego anasema taaluma nyingine zote zina viwango na mtu akishindwa kuvifikia anaondolewa katika orodha au daftari la wanataaluma lakini kwa wanahabari hali ni tofauti, “ mtu anaweza kuwa dereva wa  taxi na kesho akaitwa mwanahabari kwa sababu tu anaweza kuandika, hili ni jambo la hatari kubwa,” anasema Lutego.

Naye mhariri Deodatus Balile alisema siyo sahihi kuwashambulia tu waandishi na wahariri bali tuwajengee uwezo wa mafunzo ya usalama ndipo tuanze kuwakosoa kwa kile kinachoonekana kwamba wamekosa maadili.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhuru wa Habari Kusini mwa Afrika-Tawi la Tanzania (MISA-Tan) Tumaini Mwailenge anasema ‘njaa’ za wanahabari zisiwafanye wakaiweka rehani taaluma yao.

Akifunga mjadala huo afisa mwandamizi wa MCT, Austerius  Banzi anasema wanahabari wa Tanzania sasa wawe makini kwani kuteka, kutesa, kubaka na hata kuua ni sehemu ya siasa chafu.

================

Vidodoso kwa fikra zako msomaji

  1. Mkurugenzi aliyepita wa TBC Bwana Tido Mhando inadaiwa alinyimwa kuongeza mkataba katika wadhifa wake kwa sababu alitoa haki sawa kwa CCM na CHADEMA na vile vile kwa kuruhusu mgombea wa wa CCM, Jimbo la Ubungo, Bi Hawa Ng’umbi kudhalilishwa na wapinzani wake.
  2. Mhariri wa Daily News aliandika tahariri tena ukurasa wa mbele wakati wa Uchaguzi Mkuu, mwaka 2010, akimlenga Dkt. Slaa na kuandika Padri huyu (Slaa) hawezi kuwa rais wa tano wa Tanzania!

Tafakari mambo haya mawili katika muktadha wa mjadala wa leo


Kuporomoka majengo Dar: Tumekwama, tumeshindwa!

$
0
0

Sherehe za pasaka ziliingia dosari hususan kwa wakazi wa Dar es Salaam kufuatia kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 mtaa wa Indira Gandhi katikati ya mji. Watu wengi wamejeruriwa na vifo vimefikia watu 36.

Hii si mara ya kwanza kwa jengo kuporomoka jijini Dar es Salaam. Miaka ya hivi karibuni ilitokea huko Chang’ombe manispaa ya Temeke kwa jengo la ghorofa  nne kuporomoka na kuua watu wanne, baadae jengo la ghorofa 10 katikati ya mji liliporomoka na kuua watu watatu na hivi karibuni huko Sinza na kadiri ya mwenendo inaonyesha halitakuwa jengo la  mwisho kuanguka.!

ghorofa laporomoka dar

Ghorofa lililoanguka, mitaa ya Indira Gandhi – Dar

Nakumbuka jengo lilivyoporomoka Chang’ombe-Temeke, Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa aliamuru watu wawajibishwe na ikaundwa timu ya ukaguzi wa majengo hapa Dar es Salaam sijui iliishia wapi! Tunarudi kwenye shida ile ile. Kiufupi majengo mengi yanayoota kama uyoga hapa Dar yananitia shaka. Hivyo, suala la ukaguzi wa majengo ni muhimu; iwe kwa majengo mapya na hata yale ya zamani.

ghorofa-laanguka-sinza

Ghorofa lililoporomoka mitaa ya Sinza – Dar

Tatizo kubwa linajidhihirisha kwa kushindwa kwetu kujenga taasisi bora na imara za usimamizi sio tu katika sekta ya ujenzi lakini kwenye usimamizi wa mambo mengi tu. Kuna taasisi za kiusimamizi na watu wanaolipwa kwa mfano wa kufanya ukaguzi wa majengo ‘’wataalamu’’ lakini haieleweki wanafanya nini na likitokea la kutokea wanaanza kurushiana mpira. Ili mradi wa ujenzi wa jengo kama hilo ufanyike kuna hatua nyingi za kufuata za kiukaguzi lakini wapi! Hayafanyiki na yanayotokea ndo hayo.

Kitu kingine kinachoshangaza, haya majengo yanajengwa kweupe kila mtu anaona mjini na sio vichochoroni ukaguzi unashindwaje kufanyika, hawayaoni? Rushwa nadhani ndo inayofanya hao wakaguzi wakaweka utaalamu wao pembeni (kama wanao) na kuacha mambo yakienda ndivyo sivyo kama sio rushwa ni nini hasa? Hii pia inafungua maswali mengine na hitaji la kusimamia kimadhubuti tabia ya vitendo vya rushwa katika usimamizi ambapo vibali hutolewa pasipo stahili alimradi mhitaji wa kibali anamudu kuhonga, kununua haki ambayo hastahili kuipata! Hakika ule usemi wa; “tamaa mbele mauti nyuma” kwani tamaa fedha ya wachache inasababisha mauti ya wengi.

Nilimsikia mhusika mmoja akisema vibali vya kujenga jengo vilionyesha ni ghorofa kumi tu lakini wajenzi walikuwa wameongeza nyingine sita ambazo hata kipofu angeziona mweh!

Kuna umuhimu wa kujenga taasisi za usimamizi hapa nchi zenye weledi, uwezo, na utashi wa kufanya kazi zao kiuadilifu ili tuweze kusonga mbele. Pia kuna umuhimu wa taasisi hizo kulazimishwa kufanya hivyo na uongozi wa juu (ambao nao unatupa mashaka, ila hatuna jinsi si tuliwachagua!) la sivyo huduma kutoka kwenye taasisi za usimamizi zitaendelea kutuletea vilio ambavyo hatuvistahili kabisaa!

Shida nyingine ninayoiona ya taasisi hizi za umma ni kutokujifunza kwa yale ambayo yamekwisha likumba Taifa letu. Mifano niliyoitoa hapo juu inaadhihirisha yameporomoka majengo matatu kabla ya hili la juzi lakini kulikuwa hamna kujifunza. Wahenga wanasema; “kosa si kosa, bali kosa ni kurudia kosa”!

Kwenye ajali za meli  ilianza ajali mbaya kabisa ya MV Bukoba mnamo mwaka 1996 zikafata ajali zingine za kutisha zote kubwa na zenye kupoteza uhai wa wananchi wetu. Tumekataa kujifunza.

makaburi-mv-bukoba

Yaliyaanza mabomu Mbagala hatukukujifunza ikaja Gongo la Mboto sijui mpaka tukumbwe na nini ndo tutaamka! Hii ndiyo jamii yetu!

Juzi juzi tu tumeona vikosi vyetu vya zimamoto vilivyohangaika kuuzima moto ulioanza kwenye ghorofa moja ya juu ya jengo la PPF tower pale mjini, Zimamoto wenyewe walikiri jinsi ukosefu wa vifaa ulivyowakwamisha katika zoezi hilo ingawa walifanikiwa kuzima moto. Lakini utashangaa hali ya kikosi hicho cha zimamoto itabaki hivyo hivyo bila kuboreshwa wakati huduma yao ni muhimu kwa usalama wa watu na mali zao.

ghorofa-likiungua-kariakoo

Ghorofa likiungua mitaa ya Kariakoo

Taasisi chache au wizara zizofanya vizuri ni kwa sababu ya watu tu ‘‘personality’’ wawili watatu wanaoziongoza lakini hamna uwezo wa kitaasisi kwa kweli. Na mara nyingi watu hao wakiondoka inakuwa ni bahati nasibu kwa taasisi hiyo au wizara kuendelea kufanya vizuri. Na kwa sababu kufanya vibaya ndo imekuwa kawaida katika medani za uongozi wetu wafanya vizuri wanapingwa, kuhujumiwa na mfumo wa kiutendaji na hata kuonekana watu wa ajabu.

Tumejiwekea sheria taratibu na kanuni sisi wenyewe lakini tunashindwa kuzifuata na hiyo ndo inasababisha kukwama. Ili kuwa na taasisi imara lazima watu watii sheria na taratibu zilizowekwa, mamlaka zetu za juu za uongozi kama wizara husika lazima lisimamie hili. Kama tunayataka maendeleo lazima pia tubadilike kwa kiasi kikubwa katika namna ambavyo  tunavyoyafanya mambo yetu la sivyo tutaendelea kushuhudia majanga yenye kuweza kuzuilika yakiikumba jamii yetu

Uwajibikaji na kuwajibishana serikalini pia kungesaidia kurekebisha madudu mengi yanayotokea na hii haijalishi hata kama Waziri wa wizara husika hahusiki moja kwa moja na mambo ya hovyo yanayotokea kwenye taasisi anazoziongoza. Hii ingewafanya wawe makini zaidi na kuwabana walio chini yao kufuata taratibu zinazoongoza taasisi zao. Jambo ambalo kwa sasa hilo halipo.

Ni muhimu sana kwa kila mtu afanye kazi yake ipasavyo na awajibike mambo yakienda mrama. Kwa upande mwingine kwetu wananchi, ni kama vile tuna mioyo ya chuma yenye kuhimili kushuhudia utendaji mbovu wa viongozi na watendaji mbalimbali katika taasisi husika bila kuchukua hatua stahiki. Tumechoka kuona baada ya mambo kwenda hovyo viongozi wetu kwenye vyombo vya habari na maelezo marefu ya kuunda tume na kuahidi huo uvurundaji hautatokea tena wakati wenyewe ni sehemu ya tatizo.

Mpaka hapo tutakapobadilika na tukayakataa madudu kwenye uongozi wetu, ndio tutajikwamua kutoka hapa tulipo. Hatuoni kama viongozi wetu wanajiona kama sehemu ya tatizo wanaamini kama bado wao ni sehemu ya sululisho kama inavyotakiwa iwe kitu ambacho sicho. Ni wakati sasa wa kuwaambia kwamba wao ni sehemu ya matatizo yetu makubwa.

Poleni wafiwa na Mungu awajalie wepesi katika kuyapokea haya!

Tanzania na Ushirikishwaji wa Wananchi katika Maendeleo ya Jamii

$
0
0

Katika maendeleo yoyote yale ili yawe endelevu na yenye manufaa kama kusudio lake lilivyopangwa, kuna vitu muhimu lazima kuzingataiwa likiwemo hili la ushirikishwaji (participation of community).

Ushirikishwaji katika maendeleo ya jamii ni kitendo ambacho wale waliokusudia kuanzisha mradi wa maendeleo katika eneo fulani huwashirikisha wananchi husika (hasa wale ambao ule mradi umewalenga) ili kujaribu kupunguza vikwazo katika ufanikishaji wa mradi huo. Ushirikishwaji huo utakuwa katika nyanja kama; upangaji mikakati (strategic planning), huduma zitatolewaje, pamoja na mambo mengine yanayofanana na hayo ili mradi tu yawe yanaendeleza mradi.

Nia kubwa ya kuamua kulizungumzia hili suala ni kujaribu kufikisha ujumbe kwa wahusika ikiwemo serikali (decision makers) ili kujaribu kuangalia upya swala la ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo. Watendaji katika Serikali yetu ya Tanzania wamekuwa wavivu sana katika kuwashirikisha wananchi katika miradi mbalimabali ya maendeleo hivyo kuifanya miradi hiyo isifanikiwe kama kengo lake lilivyopangwa. Hii inawafanya wananchi kutokuwa na mipango mkakati ya kuitumia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa wakati wa utekelezwaji wa hiyo miradi. Mradi kama ‘Machinga Complex’ ni picha halisi ya jambo ninalozungumzia.

Kwahiyo, swala la ushirikiswaji linaweza kuwa chachu ya maendeleo hata kama liwe kwa muda mfupi kwa mfano jinsi TCRA walivyojaribu kuwashirikisha wananchi katika dakika za mwisho za uzimaji wa mitambo ya analojia hapa Tanzania mwishoni mwa mwaka jana (2012). Walijaribu kutoa miongozo na maelezo kwa njia tofautitofauti vikiwemo vyombo vya habari kupitia matangazo, vipindi maalum, midahalo, makala, pamoja na nyimbo kitu ambacho kiliamsha hisia za watanzania walio wengi na kuamua kuhamia digitali japokuwa kuna changamoto nyingi.

Lakini, kwa upande mwingine wananchi nao wako nyuma sana kwani hawataki kujihusisha na mambo muhimu ambayo serikali yao inawaletea mitaani kwao; wengi husingizia kuwa na majukumu mengi sana hadi kushindwa kushiriki kikamilifu katika miradi na hata kushindwa kuishinikiza serikali iwashirikishe au iitekeleze miradi kwa mujibu wa mipango mkakati.

 JE, USHIRIKISHWAJI UNA FAIDA GANI?

Faida za ushiriklishwaji ziko nyingi sana na ni muhimu kama tunataka kweli kuleta maendeleo endelevu hapa nchini kwetu Tanzania. Faida hizo zinamuelekea mwananchi moja kwa moja pamoja na serikali au wenye miradi kama ifuatavyo;

Ø  Unapunguza vikwazo kutoka kwa wananchi husika wa eneo lile kutokana na wao kuwa na uelewa na kinachoendelea na nini hatima yao mwishoni mwa mradi

Ø  Ushirikishwaji pia unaleta ile hali ya ulinzi (sense of security) pale ambapo kila mmoja anakuwa katika hali ya kuulinda ule mradi kwa sababu anajua nini hasa lengo la kile kanachotendeka pale.

Ø  Umiliki wa ule mradi unakuwa wa Jamii, kitu ambacho kitasaidia ule mradi kuwa salama na endelevu kwa kua kila mwananchi atakuwa ameutunza kama wake kutokana na ile hali ya ushirikishwaji kabla ya kuanza kwa mradi.

Ø  Ushirikishwaji pia utasaidia kufikiwa kwa lengo ambalo waandaaji wa ule mradi waliukusudia

Ø  Itasaidia pia kuzingatia swala la utamaduni wa wazawa ili kuzuia uvunzaji wa miiko ya jamii husika.

TAFAKARI: KUNA UMUHIMU MKUBWA SANA WA KUSHIRIKISHWA KULIKO HASARA JAPO KUA HAKUNA KISICHOKUWA NA FAIDA NA HASARA.

KUNA HASARA PIA KUWASHIRIKISHA

 Nazo ni

  • Kupoteza muda mwingi
  • Vipingamizi vitakuwa vingi
  • Kuna watu wengine watapuuzia

JE, NANI WAKULAUMIWA?

Kutokana na hali ilivyo sasa hasa Tanzania na nchi nyingi za kiafrika, tukimtafuta mchawi ni nani tutakamatana wenyewe na kulaumiana lakini chanzo cha tatizo haliko kwetu tu ila ni kwa dunia nzima. Ukijaribu kupitia vitabu mbalimbali vya sayansi ya jamii utabaini kuwa kuna kitu ambacho kinatutenganisha sisi na serikali yetu pamoja na wananchi wengine. Mwanasayansi ya jamii mmoja anayefahaamika kwa jina la Karl Marx alisema kuwa kupotea kwa nguvu kazi ya pamoja kumeteketezwa na mfumo wa kibepari ambao umetawala dunia kwa sasa. Naam, ubepari kimekuwa chanzo kikuu cha utengano!

Katika ubepari huwa kuna kauli moja wanaitumia ambayo inasema ‘EVERY THING IS FOR YOUR SELF BUT GOD ONLY IS FOR US ALL’ kitu ambacho kinatutenganisha sisi wote hadi hata miradi inavyoletwa  kwenye maeneo yetu tunashindwa kushirikishwa kutokana na kila mtu anakuwa akifuatilia maisha yake mwenyewe kwasababu hakuna atayemsaidia zaidi ya kumcheka na kumsengenya pale atakapokuwa amekosea.  KWA MAANA HIYO TUNAGUNDUA KUA UPEPARI UNAOIMARISHWA NA UTANDAWAZI NDIO CHANZO KIKUU CHA TATIZO HILI KATIKA NCHI YETU AMBAYO NI CHANGA BADO KIUCHUMI LAKINI IKIWA NI MOJA KATI YA NCHI KONGWE KATIKA BARA LA AFRICKA.

NINI KIFANYIKE?

Hapa watanzania na waafrika kwa ujumla inabidi tuziamshe akili zetu na tujaribu kuangalia nyuma tulikosea wapi ili tupange mikakati ambayo itaweza kutukwamua hapa tulipo.

Nikijaribu kuiangalia Tanzania kisayansi ya Jamii, kidogo nagundua kuwa mfumo wa maendeleo ambao tunautumia ni kama ule WW Rostow aliutoa katika nadharia (theory) moja ianyoitwa ‘modernization’ ambayo inatutaka ‘Ili tufikie walipofikia wenzetu wa Marekani na wa Ulaya, lazima tupitie hatua ambazo wao walizipitia ikiwa ni kutoka low stage ambayo wanaiita traditional stage, alafu tufuate hatua ya pili ambayo ni pre-condition stage, alafu tuendelee na take off stage ambayo kidogo mafanikio yanaanza kuonekana kwenye hatua hii alafu hatua ya nne ni drive to mature stage ambayo watu waanza kuwekeza katika viwanda vikubwa na hatua ya mwisho ni high mass consumption ambayo watu wanawekeza nje ya nchi zao na wanakuwa na vipato vikubwa’.

Sasa kwa sisi watanzania kweli tunafuata hizo hatua (stages) lakini tunakosea kitu kimoja ambacho kinatufanya sisi tuwe nyuma kimaendeleo. Kitu hicho ni kuwa tunafuata hatua kweli lakini mambo ambayo tunayafanya yanakuwa yamevuka ile hatua tulio nayo. Ni sawa na mtoto wa miaka mitano anaanza kuchumbia mwanamke ili kuoa.

Tumeamua kujiingiza kwenye masuala ambayo tusingetakiwa kuyaruhusu kwa wakati huu hadi pale ambapo tungekua angalau tumefikia kwenye take off ya ukweli. Hii ni kwa sababu wenzetu walifanya hivyo wakafanikiwa na kwakua hata wewe ukiendelea hutaki mwenzako akupite basi unaamua kumdanganya ili ajiingize katika mambo ambayo yatakua mzigo kwake baadaye ili uendelee kutamba; hivyo ndivyo wanavyotufanyia wazungu ili tuzidi kushindwa zaidi. Kikubwa kilicho tufanya hadi tukafikia hatua hiyo ya kujiingiza kweye mambo yasio ya uwezo wetu ni swala zima la utandawazi tulio upokea kwa kwa mikono miwili enzi za serekali ya awamu ya tatu. Wanasayansi walisha sema wazi kuwa ili utandawazi uifanikishe nchi na wananchi wake ni lazima nchi hiyo iwe na uchumi mzuri na wa ushindani zaidi ya hapo utandawazio huo unakua ni hatari.  Utandawazi huo ndio umekua chombo au silaha ya ubepari kututeganisha sisi kwa sisi na serikali yetundio maana hata ushirikiswaji wetu kwenye shughuli za maendeleo ya jamii yetu unakua haupo na kama ukiwepo unakua si wa moja kwa moja.

MAPENDEKEZO

Inabidi watanzania tuamke na tujaribu kufikiria njia sahihi ambazo tunaweza kuzitumia hasa katika mfumo huu huu wa kibepari ili kuleta maendeleo yetu wenyewe. Tunatakiwa kuishinikiza serikali kutengeneza msingi imara wa uchumi (strong economic base) ambao utatokana na rasilimali zetu tulizo nazo kama hizi za gesi na madini. tatafanikiwa hili  kwa kutowekeza muwekezaji yeyote yule isipokuwa serikali ndo iwe mmiliki na muuzaji wa hizi rasilimali ili ziwe uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu ambapo mwisho wa siku serikali hiyohiyo itakuwa imepata kipato kikubwa cha kutuendeleza sisi kuliko serikali kutegemea kodi kama chanzo cha mapato.

Ukweli unabaki kwamba bila kushirikishwa kikamilifu katika shughuli nzima za maendeleo yetu wenyewe  tutazidi kuwa masikini na ongezeko kubwa la watu wanaoishi katika mazingira magumu na matatizo mengine ya kijamii hivyo serikali inabidi ichukue hatua mahususi ili kujaribu kufanya jambo ambalo linahitajika na watanzania walio wengi hasa wa hali ya chini.

Tunachotakiwa kujifunza na kuomba kutoka kwa wachina

$
0
0

Ni miaka mingi sasa tumekuwa tunaisifu China kuwa ni nchi iliyopiga hatua kubwa kimaendeleo, na mara kwa mara wanasiasa wetu wamekuwa wakiitaja China kuwa ni nchi ya mfano wa kuigwa, hasa kutokana na yale wanayosikia kutoka kwenye vyombo vya habari na yale wanayoyaona wanapofanya ziara zao nchini China.

Ukiwa unaishi nchini China kwenyewe, ni kweli unaweza kuona kuwa neno ‘maendeleo’ ni neno lenye maana hiyo, na si neno la kufikirika tu ambalo linatoka kwenye vinywa vya wanasiasa, hasa wale wanaopenda kutumia neno hilo kama njia ya kujionesha kuwa wana nia ya kuleta maendeleo. Ukiwa nchini China (nilipo, na nimekaa kwa takribani miaka kumi sasa), kila baada ya muda fulani unaweza kuona kuna kupiga hatua kwenye maisha ya watu wa kawaida, na hata ukiwauliza watu wa kawaida, wa mjini au vijijini, wa sehemu za mashariki zilizoendelea kiuchumi na sehemu za magharibi zilizoko nyuma kiuchumi, wote wanaweza kukwambia wanaweza kuona kuwa nchi yao inapiga hatua.

Mwanzoni nilikuwa nafurahi sana nilipokuwa naona viongozi wetu wanafanya ziara nchini China, kwa matarajio kuwa wanaweza kuona na kujifunza kinachofanyika hapa China, na kukitumia kule nyumbani.

Siwezi kuweka orodha ya mawaziri na maofisa wa serikali waliofanya ziara China, wengine hata wametembelea mara kadhaa, lakini kimsingi kinachoendelea ni kilekile, hakuna kikubwa tunachoiga na kujifunza, na sababu kubwa ni kuwa hatufanyi juhudi za kujifunza, na hata hatuweki mazingira hayo. Naweza kutoa mifano kadhaa ambayo hata ninapoongea na wachina marafiki zangu huwa wananiuliza.

Ninachokiona hapa China ni kuwa wenzetu wakinunua kitu, huwa hawakifurahii tu, huwa wanaangalia kitu hiki kikoje, kina nini ndani yake, na kinafanya kazi vipi. Maana yake ni kuwa wanataka kujua ni vipi wanaweza kutengeneza kitu hicho, au hata kupata teknolojia yake, ili kesho wasirudi kulekule. Ukiangalia sisi Tanzania unaweza kuona kuwa hakuna juhudi hata kidogo za kuingiza teknolojia, hata ambazo kwa wenzetu ni ndogo na hazihitaji nguvu nyingi. Inawezekana kuwa tuna sera zinazotaja au kuielekeza serikali kwenye mambo haya, lakini ziko kwenye makaratasi tu.

Nikichukulia mfano wa barabara za nchini mwetu Tanzania, utaona kuwa kuna nyingine zimejengwa na makampuni ya kigeni, tena kulikuwa na watanzania wanashiriki kwenye kazi za ujenzi. Lakini hakukuwa na mpango wowote wa maana kukamata utaalam/teknolojia hizo, kama wachina wafanyavyo. Kwa Tanzania ujenzi wa barabara ni mradi endelevu, kwa hiyo lingekuwa ni jambo la maana sana, kama kungekuwa na utaratibu wa maana wa kuweka mazingira ya kuwa na utaalam/teknolojia hizi, leo tungekuwa tumeweza kujenga barabara nyingi tu. Ukiangalia kampuni zinazotoka Ulaya, mara nyingi huwa zinakuja na wataalamu wachache sana, huenda hawafiki hata kumi. Wengine pesa wanapata kutoka kwa serikali yetu wanajenga barabara na kujipatia faida kubwa. Kungekuwa na mipango ya maana (kama ipo, basi ingekuwa inatekelezwa), tungeweza kuwa na wataalamu 10 au hata 20 wa Tanzania wanaoweza kuchukua nafasi ya hao wageni na barabara zikajengwa.

Leo tuna mradi mkubwa wa kujenga bomba la gesi kutoka kusini kuja Dar es Salaam, gharama yake itakuwa ni zaidi ya dola bilioni mbili za Kimarekani. Tungekuwa wachina, tusingekuwa na haja ya kuagiza kampuni kutoka nje kuja kujenga bomba hili na kugharamia fedha zote hizo. Kama tungekuwa na mipango kama ya wachina kupata teknolojia wanazohitaji, ujenzi wa bomba la mafuta kati ya Tanzania na Zambia (TAZAMA) ungekuwa ni funzo ambalo lingetufanya leo tusigharamie mabilioni ya dola kujenga bomba linalofanana na jingine ambalo limewahi kujengwa Tanzania.

Sitaki kuamini kuwa katika mwaka huu na karne hii hatuna watanzania wanaoweza kufanya mambo haya, sitaki kuamini kuwa hatuwezi kuwa na idara ya kuhifadhi teknolojia ambazo tutaendelea kuzihitaji kesho na hata baada ya miaka 100 ijayo. Ni vizuri tujifunze kutoka kwa wenzetu wachina, ili na sisi tuweze kuwa na maendeleo kama wao. Utaratibu wa kuwasifia tu kila siku, wakati sisi hatufanyi juhudi, hauna tija hata kidogo!

Uzuri ni kwamba China ni rafiki mkubwa sana wa Tanzania. Kutokana msingi wa uhusiano wa nchi zetu uliojengwa na mwenyekiti Mao Zedong na Mwalimu Nyeyere, na uhusiano wa karibu kati ya Waziri Mkuu Zhou Enlai na Mzee Salim Ahmed Salim (wakati China iko kwenye harakati ya kupata kiti chake kwenye Umoja wa Mataifa), China iko tayari kutusaidia wakati wowote. Hata leo tukitaka kuomba msaada wa fedha kwa China tunaweza kupewa tena kwa masharti nafuu sana, lakini Je, ni kweli sisi ni watu wa kuomba msaada wa fedha tu kila siku? Hakuna kitu kingine cha kuomba ambacho kinaweza kutusaidia tusiende kuomba tena kesho na chenye thamani kubwa kuliko pesa? Kwanini tuisombe msaada wa teknolojia, ambazo China inazo nyingi na iko tayari kutupatia?

Hata siku moja China haiwezi kusema chukueni teknolojia hii, ina manufaa zaidi kuliko fedha mnazoomba. Utaratibu wa kuomba msaada wa fedha kila siku, na kuomba misaada ya mtindo wa “mkono uende kinywani” (si kutoka kwa wachina tu hata kutoka Ulaya na sehemu nyingine) ni aibu! Ni sawa mtu unapoenda kuomba pesa kwa mtu fulani, hujui ukiondoka nyuma yako mtu huyu atasema nini na atakusemaje mbele ya wengine, na hata ukienda kwake kesho atasema huyu mtu hakuna la maana linalomleta hapa zaidi ya kuomba pesa.

Kwa sasa kuna watanzania wengi sana wanakuja kusoma hapa China, lakini ukiangalia wanachofanya wanaporudi nyumbani ni kama wanamwagwa tu kwenye soko la ajira, na kuingia kwenye mambo ambayo huenda hayana manufaa makubwa. Kama serikali ingewatumia watu hao kisawasawa, huenda leo tungekuwa na kampuni kubwa ya kitanzania yenye uwezo wa kujenga barabara za kiwango cha juu, na hata ambayo ingeweza kupata kandarasi nje ya Tanzania. Lakini kwa sasa bado hatuna “coordinated efforts” za kunufaika.

Kama tukiendea na hali hii tutaendelea kutumia pesa nyingi kufanya yale ambayo tunaweza kuyafanya kwa robo ya gharama. Ni wakati wa viongozi wetu Tanzania kubadilika, kwa manufaa ya watanzania na vizazi vyetu vijavyo!

Kinachosemwa, na Ukweli kuhusu Sera ya Mtoto Mmoja nchini China

$
0
0

Sera ya uzazi wa mpango ya China, maarufu kama sera ya mtoto mmoja, ni sera inayofahamika sana duniani kwanza kutokana na ufanisi wake katika kudhibiti ongezeko la idadi ya watu, na pili kutokana na kupata upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya taasisi za kidini nje ya China. Lakini pamoja na sera hiyo kufahamika kutokana na sababu hizo mbili, bado watu walio nje ya China wana uelewa mdogo sana kuhusu undani wa sera hii, na hawajui inatekelezwa vipi, ina manufaa gani na changamoto gani, na nini tunaweza kujifunza kutokana na sera hii.

Sera ya uzazi wa mpango ya China ilianza kutekelezwa miaka 70 karne iliyopita, ili kudhibiti ongezeko la kasi la idadi ya watu. Kimsingi sera hii inawataka kila wanandoa wachina wawe na mtoto mmoja. Nimeamua kutumia neno “kimsingi” kwa kuwa si wanandoa wote wanaotakiwa au wanaolazimishwa kuwa na mtoto mmoja kama baadhi ya watu wanavyoambiwa na kuamini.

Sera hii kwanza inawalenga watu wa kabila kubwa zaidi la China, yaani wa-Han, ambao wanachukua zaidi ya 95 ya idadi ya watu wote wa China. Watu wa makabila mengine ambayo nchini China yanaitwa makabila madogo madogo wanaweza kutekeleza sera hiyo kwa hiari, na baadhi yao hata wanapewa ruzuku kutokana na kufuata sera hiyo kwa hiari. Hata hao wa-han si wote wanaotakiwa kutekeleza sera hiyo kama sera inavyoelezwa, kuna wakati baadhi hawabanwi sana na sera hiyo.

Kwa mfano, wa-han wachina wanaoishi vijijini wanaotegemea shughuli za kilimo, sera hii haiwabani sana kwa kuwa wanahitaji nguvu zaidi, kwa hiyo wanaweza kuwa na mtoto zaidi ya mmoja. Wa-han wa mijini ambao wote ni mtoto pekee kwenye familia zao, wakioana wanaruhusiwa kuwa na watoto wawili. Wa-han wanaobanwa na sera hii wakienda kinyume wanatozwa faini. Kwa hiyo ukiangalia vizuri unaweza kuona kuwa, kwa wachina wa kabila la wa-han sera hii ni kama sheria, lakini kwa wachina wa makabila mengine ni sera ambayo utekelezaji wake ni hiari.

Hebu kwanza tutupie macho hali nchini China katika miaka ya 1970 wakati ilipoamua kutekeleza sera ya uzazi wa mpango. Jamhuri ya watu wa China ilianzishwa mwaka 1949 baada ya mapigano na vita vilivyodumu kwa karibu miaka 100 nchini China. Mwaka 1949 idadi ya wachina ilikuwa milioni 550, na kwa wastani watu waliokuwa wanaishi miaka 35. Lakini hadi kufikia mwaka 1980, idadi ya watu wa China iliongezeka na kufikia bilioni 1 na umri wa wastani wa maisha ya mchina pia uliongezeka na kufikia miaka 68. Kutokana na makadirio yaliyofanyika mwaka 1980, idadi ya watu wa China ingeweza kufikia bilioni 1.4 hadi ifikapo mwaka 2000.

Ukiangalia sababu nyingi zilizowafanya wachina waanze kutekeleza sera hii, unaweza kuona kuwa kuna mazingira mengi yanayofanana na hali ya sasa ya Tanzania. Idadi kubwa ya watu ni shinikizo kubwa sana kwa maliasili na raslimali za jamii kama vile ardhi, maji, chakula, shule, hospitali na miundo mbinu mingine. Mwanzoni mwa miaka ya sabini changamoto hizo zilikuwa ni mzigo mkubwa sana kwa wachina, na ni changamoto hizo hizo ambazo kwa sasa sisi watanzania tunalalamika nazo kila kukicha. Lakini changamoto hizo hazipo kwa Tanzania peke yake, bali pia zipo katika maeneo mengine duniani, ambako maliasili zinaendelea kupungua.

Nchini China watu walijua kuwa kama wakiendelea kuzaliana kwa wingi, basi ingekuwa ndoto au ingechukua muda mrefu kuwa na ongezeko la uchumi, na hata kama kungekuwa na ongezeko lolote la uchumi, ongezeko hilo lingefutwa na ongezeko la idadi ya watu. Kwa sasa hapa Tanzania tunasema kasi ya uchumi wa nchi yetu inaongezeka kwa asilimia zaidi ya 5 na 6 hivi. Hii kwa kweli ni habari nzuri, lakini ongezeko hilo halionekani kwenye maisha ya mtanzania wa kawaida, inawezekana kuwa ongezeko hilo linafutwa na ongezeko la idadi ya watu.

Hata tukiangalia familia moja moja, ni wazi kuwa ukiwa na watoto wengi kuliko uwezo wako wa kuwamudu, kwanza kama mzazi utatumia muda mwingi kujaribu kuwatunza watoto wako, na pili unaweza kukosa muda wa kutosha kutumia akili zako na nguvu zako kufanya mambo mengine yanayoweza kukunufaisha wewe na kulinufaisha taifa.

Mbali na maelezo yanayotolewa na serikali ya China kuhusiana na manufaa ya kiuchumi yanayotokana na utekelezaji wa sera hii, ukiwauliza wachina wa kawaida hasa wa mijini, wanakwambia kuwa hata kama isingekuwa sera ya serikali, wengi wao wanalazimika kutekeleza sera hiyo kutokana na mazingira ya sasa ya kiuchumi. Si rahisi kumudu kununua nyumba ya kuwatunza watoto watano, si rahisi kununua chakula cha kuwalisha watoto wengi namna hiyo, na zaidi ni vigumu sana kumudu gharama za elimu, matibabu na huduma nyingine kwa ajili ya watoto. Kwa ufupi ni kwamba, kuwa na idadi kubwa ya watoto, kwa mazingira ya nchi kama China, hasa mijini, ni kujiletea matatizo makubwa.

Hata hivyo sera yoyote lazima iendane na hali halisi. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na ongezeko la uchumi na kuinuka kwa kiwango cha maisha, wachina hasa wakazi wa mijini katika maeneo yaliyoendelea kiuchumi, wanandoa vijana wanaonesha nia ya kuahirisha umri wa kuzaa mtoto, na baadhi yao kuamua kutooana au kutozaa.

Kwa upande mwingine wazee wanaishi kwa muda mrefu zaidi, hali ambayo inafanya kuwe na wazee wengi katika jamii ya China. Ndiyo maana pamoja na kuendelea na juhudi za kudhibiti ongezeko la kasi la idadi ya watu, serikali ya China imeanza kufikiria na kuchukua hatua ya kurekebisha sera yake ya uzazi wa mpango. Hatua moja ni kwamba, wanandoa ambao wao ni mtoto pekee kwenye familia, wanaruhusiwa kuwa na watoto wawili. Na serikali pia ilichagua baadhi ya maeneo kufanya jaribio la watoto wawili, lakini watu wengi waishio maeneo hayo hawapendi kuzaa mtoto zaidi ya mmoja, tofauti na ilivyodhaniwa. Kuna wachina wengi tu ambao wanaamua kuoana na kutozaa, labda kutokana na utamaduni wa sisi waafrika jambo hili halifikiriki.

Pamoja na kuwa sera hii imeshambuliwa na jumuiya za haki za binadamu duniani na taasisi za kidini, hasa kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya utoaji mimba hasa inapojulikana kuwa ni mtoto wa kike, na kutokana na kinachotajwa kuwa ni kuzuia uhuru wa mtu kuamua idadi ya watoto anaotaka, lakini tukiangalia lengo la kimsingi la uwepo wa sera hii—kulinganisha matokeo ya uzalishaji wa mtu mmoja moja na thamani ya uzalishaji wa mali na maendeleo ya uchumi na jamii kwa ujumla, tunaweza kusema sera hii kimsingi imekuwa na manufaa kwa mtu mmoja mmoja, familia na nchi kwa ujumla.

Inakadiriwa kuwa sera hii imepunguza ongezeko la idadi ya watu kwa watu milioni 400, maana yake ni kuwa maliasili na rasilimali ambazo zingetumika kwa ajili ya watu hao milioni 400, sasa zinatumika kuboresha maisha ya watu waliopo sasa. Afya ya kina mama wanaojifungua na huduma wanazopata wakati wa kujifungua vyote vimeboreshwa, na kutokana na kutokuwa wajawazito mara kwa mara, kina mama wanashiriki zaidi kwenye shughuli za uchumi, na hata watoto wanakuwa na afya zaidi, mazingira mazuri zaidi ya elimu na hata kuwa na mustakbali mzuri zaidi.

Tanzania tumewahi kuwa na kampeni kubwa iliyokuwa inatoa mafunzo mazuri sana kuhusu afya ya uzazi na hata manufaa yake kwa mlengwa, ikishirikisha taasisi zisizo za kiserikali. Pamoja umuhimu wake, kampeni hiyo ilikosolewa na baadhi ya taasisi za kidini, lakini ilionesha mwelekeo mzuri. Sijui kwa sasa Chama Cha Uzazi wa Mpango na Malezi bora UMATI kilichokuwa kinahimiza kampeni hiyo kinachukuliwa vipi, kina mwelekeo gani na kina uwezo gani wa kuhimiza upangaji wa sera za taifa kwenye mambo ya uzazi na kusimamia utekelezaji wake. Kama Chama hiki kikipewa msukomo zaidi wa kufanya kazi na kuwafikia watanzania wengi, kuna uwezekano kuwa chama hiki kitakuwa ni jibu la tatizo la ongezeko la idadi ya watu Tanzania. Kwa kuwa chama hiki kinajua vizuri mazingira ya watanzania kiuchumi, kidini na hata mienendo ya uzazi ya watanzania.

Hapa Tanzania changamoto ya idadi ya watu, haitazamwi kwa umakini unaostahili. Pamoja na kuwa kuna baadhi ya watu wanazungumza suala hilo, inaonekana kuwa lipo vinywani tu. Bado baadhi yetu tunaamua tu kuzaa kwa kuwa tumefikisha umri fulani, sio kwa kuwa kweli tunahitaji kuwa na watoto, uwezo wa kukabiliana na majukumu ya kuwa na mtoto au sisi wenyewe kuwa wazazi, au tunaiga mkumbo na kuchagua kuwa na idadi ya watoto tunaopenda kuwa nao bila kuzingatia kama tuna uwezo wa kuwatunza na kuwawezesha waishi maisha bora, na baadhi tunachukulia fahari na kuona ni jambo la kawaida kuwa na watoto nje ya ndoa, kuwatelekeza na kuwafanya wengine wawe watoto wa mitaani. Ni kawaida kuona mtu ana watoto watano, lakini kimsingi hana hata uwezo wa kiuchumi wa kumudu kumtunza mtoto mmoja, lakini ukiuliza ni kwanini ana watoto wengi, huwezi kupata jibu la maana, zaidi ya kusema Mungu atawaangalia.

Sera ya mtoto mmoja ya China ina dosari zake, na wachina wenyewe wanajua dosari hizo, na kwa sasa kuna mjadala unaoendelea kuhusu kuifanyia mabadiliko sera hiyo ili iendane na mazingira ya sasa. Siwezi kusema kuwa sera hiyo inafaa kwa Tanzania au la, kwa kuwa kuna mambo mengi yanaoendana na sera hiyo ambayo yako kinyume kabisa na maadili, utamaduni na mazingira ya Tanzania. Lakini pia kuna mambo mengi yaliyomo kwenye sera hiyo, ikiwa ni pamoja na mantiki ya sera yenyewe, yanayoweza kuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania na watanzania.

Ni bora kuwepo na sera ya maana inayotekelezwa na kulalamikwa, kuliko kutokuwa kabisa na sera au kuwa sera midomoni na kwenye makaratasi tu, na kuacha ongezeko la idadi ya watu liendelee kuwa bomu linalokaribia kulipuka.

Tunachotakiwa kukumbuka ni kuwa, sera inayohusu idadi ya watu ni sera muhimu kwa taifa inayopaswa kupangwa kwa uangalifu sana tangu mwanzo, kwani athari au manufaa yake hayaonekani mara moja, lakini hakika sera ya namna hiyo inaweza kuwa na manufaa kwa taifa pamoja na mwananchi mmoja mmoja baada ya miaka 10 hadi 20, wakati watu wa kizazi kimoja watakapokuwa wamekua, kuingia kwenye soko la ajira na kutaka maisha bora.

Watanzania zaidi ya 100 wako gerezani nchini China kuhusiana na dawa za kulevya, 20 ni wanawake!

$
0
0

Kama kuna jambo ambalo linaichafua Tanzania katika jukwaa la kimataifa kwa siku hizi, basi ni tatizo la usafirishaji wa dawa za kulevya.

Zamani tatizo hili halikuwa kubwa sana, ni mtanzania mmoja mmoja sana alikuwa akikamatwa nje kwa kusafirisha dawa za kulevya. Kwa hiyo jina la nchi yetu lilikuwa linasikika mara moja moja sana au kwa bahati mbaya kuhusiana na tatizo la dawa za kulevya. Lakini katika siku za hivi karibuni tumesikia kuwa kuna watanzania wanakamatwa Ulaya, Amerika Kaskazini, Amerika Kusini, Asia na hata katika nchi za Afrika, kama ilivyotokea majuzi huko Afrika Kusini. Kwa sasa ukisikia jina la Tanzania linatajwa kuhusiana na tatizo la dawa za kulevya, si bahati mbaya tena na si mara moja moja kama zamani.

Serikali yetu imekuwa ikijitahidi sana kujenga jina zuri la Tanzania na kuitanganza Tanzania kuwa ni kisiwa cha amani, nchi yenye vivutio vingi vya utalii na yenye ukarimu kwa wageni. Na kweli kama ukitembelea nchi yoyote yenye watu wanaoifahamu Tanzania, si vigumu kusikia Tanzania ikisifiwa, lakini kama ukiona mtu amekaa kimya, basi ujue kuna uwezekano kuwa hataki kutaja suala la dawa za kulevya.

Mwanzoni nilikuwa naamini kuwa watanzania ni watu wenye maadili ambao wanapokwenda nje ya nchi wanakumbuka kuwa “mabalozi wazuri” wa nchi. Lakini baada ya kutembelea sehemu mbalimbali duniani, hasa nchi za Asia na Asia Kusini Mashariki, na kukutana na wenyeji na kuwauliuza mtazamo wao kuhusu Tanzania na watanzania, nikagundua kuwa sifa zote nzuri za Tanzania zinafunikwa na sifa mbaya moja au mbili. Kubwa ni tatizo la dawa za kulevya, na nyingine ni ukahaba (Hong Kong).

Pamoja na kuwa ni watanzania wachache sana wanaosafirisha dawa za kulevya, ni hao wachache ndio wanaofanya jina la watanzania wengine walio wengi lichafuke, na kuwafanya watanzania wanaokwenda nje ya Tanzania kwa malengo halali, kama vile biashara, michezo na hata utalii, wakumbwe na matatizo wasiyostahili.

Zamani nilikuwa ninakasirika sana ninapotolewa kwenye mstari wa uwanja wa ndege na kuanza kupekuliwa na kuulizwa maswali ‘ya kipuuzi’, kana kwamba mimi ni mhalifu au mtuhumiwa wa uhalifu. Nilikuwa najihisi kuwa mimi ni mhanga wa ubaguzi wa rangi, kitu ambacho sikutegemea kutoka kwa nchi marafiki zetu. Kuna wakati hata nilifikia hatua ya kukwaruzana na maofisa wa uwanja wa ndege, kwa kuona wananitendea isivyostahili. Lakini baadaye baada ya kuangalia hali halisi na kuona matendo yanayofanywa na baadhi ya watanzania wanaokuwa nje ya Tanzania, nikagundua kuwa wasiwasi walionao maofisa wa viwanja vya ndege vya nchi za Asia kuhusu watu wenye pasi za kusafiria za Tanzania, ni wa haki na unaeleweka, si ubaguzi wa rangi na si ubaguzi dhidi ya watanzania. Kama ni ubaguzi wa rangi, basi matendo ya baadhi yetu ndio yanawapa kisingizio cha kufanya hivyo.

Kinachonifanya nisione kuwa ni ubaguzi wa rangi ni kuwa, nchini China kwa mfano kuna adhabu kali sana kwa watu wanaokamatwa kwa makosa ya dawa za kulevya, wachina wengi wamehukumiwa adhabu ya kifo. Lakini cha ajabu ni kuwa watanzania wanaokamatwa kwa makosa sawasawa na wanayofanya wachina, wanapewa vifungo virefu na adhabu ya kifo, lakini hadi sasa hakuna mtanzania aliyenyongwa ikilinganishwa na wachina na wafungwa wa mataifa mengine.

Kumekuwa na habari za kupotosha kwenye baadhi ya vyombo vya habari vya Tanzania kuhusu jambo hili, lakini ukweli ni kuwa Mpaka sasa hakuna mtanzania aliyehukumiwa adhabu ya kifo kwa makosa ya dawa za kulevya na adhabu yake kutekelezwa. Ni vigumu kujua ni kwanini China haijawanyonga watanzania, lakini ukiangalia sababu ya wachina kutowachukulia hatua kali watanzania, utaona kuwa wanathamini sana urafiki uliojengwa na viongozi wetu, hasa mwalimu Nyerere na mzee Salim Ahmed Salim. Kwa hiyo ukiona jinsi wenyeji wanavyochukuliwa hatua kali, na sisi watanzania “kudekezwa”, hata ukikutana na vitendo vinavyokukosesha raha unapopita uwanja wa ndege, basi inabidi uwe mpole mara moja.

Pamoja na kuwa kila suala la dawa za kulevya linapotajwa, utakachoona kwenye vyombo vya habari ni kuwa kuna mtandao mkubwa wa siri, lakini ni kama tunapuuza madhara yanayoletwa na jambo hili kwa uhusiano kati ya nchi yetu na nchi nyingine, na usumbufu linaoleta kwa watanzania wengine wasio wasafirishaji wa dawa za kulevya.

Inasikitisha kuona kuwa kati ya watu kutoka nchi za Afrika Mashariki, ni watanzania ndio wanaokamatwa zaidi na dawa za kulevya kuliko wale wakenya na waganda. Na hata watanzania wanaokamatwa, wengi wanatoka katika Mikoa miwili ya pwani, ambako baadhi ya vijana wanaona ni “ujiko” kusafirisha dawa za kulevya. Ukiongea na vijana hao, unaweza kuona kuwa hawana elimu hata kidogo, kwani hata uwezo wao wa kuandika kwa Kiswahili na uwezo wa kuongea Kiswahili na kujenga hoja ni mdogo sana, ndio maana inaonekana ni rahisi kwao kurubuniwa kuliko vijana wa Kenya, Uganda na wa nchi nyingine za Afrika Mashariki. Wengi wao wanasema wanaahidiwa kati ya dola elfu mbili na elfu nne wakifikisha “mzigo” salama. Kwa kweli hizo si pesa nyingi ikilinganishwa na hatari ya kazi yenyewe, na hasa ukizingatia kuwa kwa mtanzania anayejituma kufanya kazi nyumbani, anaweza kupata pesa hizo.

Kwa hapa China, mpaka sasa naweza kusema kwa sasa tatizo limefikia kiwango cha kutia hofu, na hasa kwa Hong Kong na Makau ambako kuna wafungwa zaidi ya 100 wa kitanzania. Tofauti na siku za nyuma, idadi ya wafungwa wa kike inazidi kuongezeka siku hadi siku ambapo kwa sasa kuna wafungwa wa kike zaidi ya 20 katika magereza ya China bara na Hong Kong. Kutokana na hali hiyo nina wasiwasi kuwa huenda ile hadhi ya watanzania kuingia katika miji hiyo bila Visa huenda iko mashakani. Lakini vigumu kwangu kama mwandishi wa habari kujua undani wa tatizo hili. Ninachojua ni kuwa kuna watanzania wengi wako gerezani, kutokana na kukamatwa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.

Niliwahi kumuuliza aliyekuwa balozi wa Tanzania hapa China na balozi wa sasa kuhusu athari ya tatizo hili kwenye uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania, wote walioonesha kukasirishwa na kusikitishwa na jambo hilo, na kusema linatia aibu. Lakini mabalozi hao hawajui ni nani anayewatuma watanzania wanaokamatwa na dawa za kulevya. Waliokamatwa nao hata siku moja hawataji ni nani aliyewatuma, wao ni kama watu waliokula yamini ya kutosema lolote, hata kama wanapewa adhabu ya kifo. Hata hivyo, wafungwa wanaeleza tu kwamba “Kuna mtandao mkubwa ambao unahitaji ushirikiano mkubwa kupambana nao, zinakopelekwa na zinakotoka dawa hizo”.

Hivi karibuni tumesikia alichokifanya Dk Mwakyembe kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere, yeye anaona kuwa uwanja unaobeba jina la Mwalimu Nyerere haupaswi kuhusishwa na dawa za kulevya. Alichofanya Dk Mwakyembe pale uwanja wa ndege kwa kweli ni jambo zuri, na kama asingefanya hivyo huenda watanzania tungeendelea kuwa kizani kuhusiana na mambo yanayoweza kuwa yanaendelea katika forodha zetu. Lakini tukiangalia kwa undani tunaweza kuona kuwa, kama uhalifu huo unatokea kwenye uwanja wa ndege unaotakiwa kuwa na usalama mkali, hali ikoje kwenye forodha nyingine mbali na ile ya uwanja wa ndege wa mwalimu Nyerere ambako hakuna kamera za video, ambako Dk Mwakyembe hawezi kwenda kwa ghafla? Kuna Namanga, Holili, Horohoro, Silari, Tunduma nk, hali ya huko ikoje? Dk Mwakyembe anatakiwa kuhakikisha kuwa kilichofanyika katika Uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere kifanyike katika forodha zote. Dk Mwakyembe analia na jina la Mwalimu Nyerere, lakini ni vizuri watanzania wote tukikumbuka kuwa tunatakiwa kulia na jina la nchi yetu, Tanzania.

Kama hali hii ikiendelea inaweza kufika hatua kuwa wanafunzi, wafanyabiashara, wanamichezo, wagonjwa na hata watalii kutoka Tanzania wanaokwenda nje ya nchi, wote watawekwa kwenye kundi la washukiwa wa biashara ya dawa za kulevya.

Wanaume: Baadhi ya sababu ambazo huwafanya wengi waogope kuingia kwenye ndoa

$
0
0

Vijana wengi wa kiume hujikuta katika wakati mgumu kuchukua maamuzi ya kuishi na mwanamke japo yawezekana wakawa wanatamani kufanya hivyo kwa muda mrefu kutokana na vikinza vingi, vingine vikiwa ni vya kimaisha na vingine ni nadharia tu.

Katika bandiko hili, nitagusia sababu kadhaa zinazochangia vijana wengi kujikuta wakisuasua au kuogopa kuingia kwenye ndoa.

Kupanda kwa gharama za maisha

Kigezo hiki huwakumba zaidi wanaume ambao wanaishi mijini. Gharama za maisha zimepanda sana kiasi kwamba mtu anaweza kuwa anaishi peke yake na bado kuna mambo ambayo anashindwa kuyatimiza kwa wakati, kama vile kozi ya nyumba, pesa ya kujikimu na mengine mengi. Wengi huona ni heri kuwa na mtu tu ambaye ni mpenzi wake kuliko kudhibiti kabisa kwa kuwa na huyo mtu kwa kuishi naye kwa hofu ya kushindwa kutimiza wajibu. Ndio maana kwa wale ambao hupata akina dada ambao wanajiweza kujitegemea na hivyo ni hodari kwa kusaidiana katika mambo ya kila siku hasa katika masuala ya maendeleo huwa wepesi kuchukua maamuzi ya kuoa.

Utitiri wa wanawake wanaopatikana kirahisi bila hata kuoa

Ni suala ambalo lipo wazi hasa maeneo ya mijini akina dada/mama wa kuwa nao katika mahusiano (bila kujalisha ni wa muda mfupi ama mrefu) wamekuwa wengi, rahisi kuwapata, wa kila aina mwanaume watakao.  Kuna wanaume wamejikita katika hilo kiasi kwamba mradi tu atake mwanamke atatoka/atatumia namba alizohifadhi kwenye simu na atafanikisha hiyo azima yake ndani ya siku hiyo hiyo ambayo amedhamiria bila shida yoyote. Hii inafanya kwa kiasi kuchangia kwa wanaume kusuasua katika maamuzi ya kuoa. Kwa kimombo hujiambia, “If I can get it for free, why buy it?”

Maradhi hasa ugonjwa wa UKIMWI

Pamoja na kuhamasishwa kwingi na wataalamu wa maradhi ya HIV/AIDs kuwa mtu hata ukiwa umeathirika unaweza kuwa na mahusiano na hata kuoa na kuwa na watoto; bado haisaidii sana kwa vijana wanaojitambua kuwa ni waathirika wakiwa bado ni wadogo, hawajaoa/olewa ama kuwahi kuwa na mtoto.  Wengi sana hukata tamaa na huona ni kheri kubaki walivyo kuliko kuingia katika ndoa. Naomba izingatiwe kuwa si wote; wengine huwa hodari na huoa/olewa saa nyingine bila hata kumjulisha mpenzi wake huyo kuwa yeye ana virusi chanya vya UKIMWI (HIV +ve).

Kufurahia ‘uhuru’

Hawa ni makapera wazoefu (wengine husema ‘bachela sugu’), hakuna mtu ambaye anaweza mshawishi akabadilisha maisha yake hayo ya kikapela (bachelor). Miaka huzidi kukatika hadi anafika miaka takribani 40 au zaidi wala hana mpango wa kuoa na wala hajutii maamuzi yake hayo. Mara nyingi wanaume wa namna hii hupenda sana wanawake (siyo lazima kuwa atawachanganya kwa kuwa na zaidi ya mmoja); huwa na uwezo (hata kama sustainable); Hutaka wanawake wadogo (mtu mzima sana kwake hapana hata kama yeye ni mtu mzima); Ni mtu wa starehe sana, haoi kamwe na hufurahia uhuru huo kwa hisia kuwa akioa ataupoteza uhuru wake.

Uhaba wa wanawake wanaofaa kuolewa

Na hii hutokea hasa kwa maeneo ya mijini. Wadada/mama wengi wamekuwa ni ‘wa mjini’ mno, wajanja, malengo mbele ikiwa imeambatana na tamaa, wanaoweka pesa mbele utu nyuma, wachanganyi (kuwa na bwana zaidi ya mmoja). Haya mambo yamekuwa yakifanywa bila kificho, inamfanya mwanaume anapokuwa katika mahusiano ahisi kuwa hata mtu wake ana tabia hizo hizo hata kama siyo kweli. Hii inakatisha tamaa kwa wanaume wengi na kuona wanawake wanaofaa kuoa (tokana na viwango vyake alivyoweka) ni adimu ama hawapo kabisa!

Kutopata ampendaye kwa dhati

Kuna wanaume vigezo vya mwanamke awe vipi havina umuhimu kabisa katika kutaka kuamua kuoa. Yeye kikubwa anataka ampate mwamake ambaye atampenda kwa dhati na huku akiwa na matumaini kuwa huyo mwanamke atampenda na yeye pia kwa dhati.  Huyu mwanaume anaamini msingi bora wa ndoa ni mapenzi ya dhati kati ya yeye na mkewe basi! Hana haraka hadi pale atakapompata mwanamke akampenda. Kama huyo mwanamke atakubali kuolewa ama lah; hilo ni suala jingine! 

Mahusiano mabovu ya awali

Kuna wanaume huchagua wanawake kwa sifa ambazo anazijua yeye mwenyewe. Yeye hamuangalii mwanamke kama mtu, bali anamuangalia kama kitu. Daima vigezo vyake ni nataka mwanamke wa hivi, tabia za vile, muonekano wa kule na mambo mengine kedekede. Hivyo unakuta kila siku yuko katika mahusiano na mwanamke ambaye ni kweli anampenda kimuonekano; ila linapokuja suala la tabia wanashindwana kabisa. Anaachana nae kisha anatafuta mwingine kwa mtindo uleule – mwisho wa siku analaumu wanawake wote ni sawa na kukata tamaa ya kuoa ama kusuasua katika maamuzi ya kutaka kuoa.

Kutoridhika na kipato chake

Kuna mwingine anaweza kuona kutoridhika na kipato (ni sawa na sababu ya kwanza niliweka ya “Kupanda kwa gharama za Maisha”) – lakini hii ni tofauti kidogo. Hapa namaanisha pale ambapo mwanaume ana uwezo kabisa wa kuwa na mke na pia kuweza kukimu mahitaji yote pamoja na ya familia yake. ILA kwa mipangilio yake anaona yeye bado; mara nyingi wa hivi anataka ahakikishe ana uwezo wa kutosha ili aweze kuishi maisha ya kifahari na si ya kujitosheleza tu. Hivyo katika hali ya kawaida ana uwezo wa kuwa na mke lakini kwa maisha ya mtu wa kawaida na si wa kitajiri kama malengo yake.

Malezi na Makuzi

Dhana mbovu juu ya ndoa

Dhana ya ndoa inaenda ikibadilika… Kumekuwa na tabia ya watu kukatisha tamaa kwa kutoa vigezo, sababu, hadithi juu ya ndoa ambazo ni za kubomoa kuliko kujenga. Sijui hawa watu hutumia vigezo gani… HATA siku moja usitarajie uishi na mtu miaka nenda miaka rudi kitanda kimoja, nyumba moja msigombane, kusiwe na madhaifu na pia kusiwe na wakati ambao wote hadi kiwango cha kukata tamaa. Ndoa ni zaidi ya starehe na kufurahi… Inahitaji nguvu kubwa, nguvu ya ziada, hekima, busara, kujituma na pia kuwa committed kwa ndoa kuweza kufanikiwa. Sisemi kuwa lazima zote zitafanikiwa maana kuna mambo ambayo yana mpaka – kuna wakati you just let go. Ila hakuna haja ya kuibomoa hiyo taasisi kwa makusudi, taasisi ambayo ni msingi bora wa malezi ya watoto kuliko taasisi yoyote ile inayoweza lea watoto ambao hasa ndiyo tegemeo la vizazi vijavyo.

Kuzaa ovyo/Kuzaa kabla ya ndoa

Kuna wanaume wanazalisha balaa! Bila kujalisha hizo mimba ni zao kweli ama wamesingiziwa kinachojalisha na watoto hao kawakubali na anawalea. Kuna wanaume hadi anafikia umri wa miaka 30 tayari ana watoto wa wanawake tofauti hata watano na analea. Kwa kiasi fulani, hii inaweza mvunja morali ya kutaka kuoa, anaona kama watoto tayari anao na anawalea hivyo hakuna haja ya kuwa na mwanamke kabisa ndani kama mke. Hii ni mara chache.

Kukua kwa idadi ya wanawake wanaotoka nje ya ndoa

Maadili mengi ya wanandoa yamezidi kushuka… Hapo nyuma ilishazoeleka wanaume huwa na tabia ya kutoka nje ya ndoa na wanawake kwa uchache. Bahati mbaya siku zinavyozidi kwenda idadi ya wanawake wanaotoka nayo inakuwa kwa kasi, tabia ambayo inafanywa bila kificho kabisa na imekuwa kana kwamba ni mashindano ya kutoka. Ni wazi thamani (reputation) ya mwanamke ambaye anatoka na mwanaume anayetoka ni tofauti. Ni wanaume wachache wana kifua cha kuweza kuvumilia mkewe/mpenziwe kutoka nje na kuendelea kuwa naye. Kwa wanaume wengi ambao hawajaoa hili huchangia katika kukata tamaa ya kupata mwanamke ambae anafaa kuwa mke na asiyeweza kuwa msaliti.

Usikose kufuatana nami katika makala yajayo!

Kilimo si kwanza: Mipango sawa, vitendo hakuna!

$
0
0

Ukizunguka vijijini ambako ndiko hasa kilimo kinaendeshwa, unaweza kustaajabu na kujiuliza endapo bado upo katika nchi ile ile yenye mipango na mikakati mingi yenye kuvutia na kauli mbinu za kila namna. Uhalisia ni tofauti sana na kinachohubiriwa. Kilimo kimepewa kisogo, mkulima ametelekezwa na kusahauliwa kabisa. Huo ndio ukweli mchungu.

Ni aibu na simanzi kuona mpaka karne hii wakulima ambao wana utashi na ari ya kushiriki katika shughuli za kilimo (ikiwemo ufugaji na uvuvi) wanakosa pembejeo za kilimo. Licha ya fedha zao mkononi; bidhaa haimo madukani. Hata uwepo wa maduka ya zana za kilimo na mifugo vijijini ni kitendawili.

Na mahala ambapo kuna maduka, tunadiriki kuleta pembejeo feki. Tunadiriki kufanya ufisadi katika pembejeo! Na zaidi kukosa uongozi wa kuhakikisha pembejeo na zana za kilimo zinaenda sambamba na msimu wa kilimo chenyewe! Bado tunaibuka usingizini na kughani matamanio tusiyoweka katika uhalisia wa kupata matokeo makubwa sasa!

Ni kweli, kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na juhudi za dhati na matamanio ya kiserikali ya kuimarisha kilimo. Lakini kwa kiasi kikubwa zinagonga mwamba. Bado rushwa na wizi vimekithiri katika pembejeo za kilimo zinazoelekezwa kukwamua kilimo huku viongozi wakiangalia au kushiriki katika dhuluma hiyo.

Viongozi wanaona soni kusimama na kumtetea mkulima, kutetea haki ya mvuja jasho anaowafanya washibe. Hakika ule usemi wa; “aliyeshiba hamjui mwenye njaa” unajidhihirisha katika watawala wetu. Ndiyo, ni watawala na si viongozi tena kwa kukosa kujali wale ambao wanapaswa kuwapigania.

Ni kweli; kumtetea mkulima yahitaji uimara hasa kwa jamii inayoongozwa na wanaojiita "watoto wa wakulima" ambao wamesahau wakulima ila makini katika kukumbuka kupiga. Wenye uthubutu wakukiri hadharani tena katika mhimili mtukufu kuwa wameshachoka (sijui wamechoka kuongoza?) na hivyo; "wapigwe tu"!

Na huko ndiko ziliko fikra, nguvu na maarifa yao wanayaelekeza (kupiga) na kusahau kuhakikisha kuwakwamua wakulima ambao ndio wengi nchini na wenye kuishi katika hali duni.

Hao ni wao; ila kila mwananchi anapaswa asijisahau. Tunapaswa kutowasahau wakulima, wafugaji na wavuvi. Shibe yetu ni kutokana na jasho na kazi ngumu wazifanyazo kila uchao katika mazingira magumu sana.

Licha ya changamoto na ugumu huo wote wanaendelea kuzalisha, bado hawafanyi mgomo wa kulima au kufuga. Au hata kuamua siku kugoma kuuza mazao yao; tena hasa kuwauzia wananchi katika miji mikuu.

Lakini kila uchao tumewapa kisogo. Hatujali hata kuimarisha upatikanaji wa zana na pembejeo za kilimo ili tuweze kuzalisha na kupata zaidi na zaidi ambacho ndicho kitufae sote na kupata  shibe.

Tuchukue mfano; asasi zisizo za kiserikali (AZAKI) mbalimbali ambazo zina uchache wa kibajeti kulinganisha na bajeti ya taasisi za kiserikali husika zinaweza kuwasimamia na kuwasaidia wakulima na wafugaji kwa kiwango cha kupigiwa chapuo. Kwanini? Hapo kuna funzo kuu! Msingi si udogo wa bajeti bali ni udhihilishwaji wa dhamira, ari na msukumo unaowekwa na watendaji na viongozi katika kuhakikisha ustawi na kukuwa kwa kilimo na ufugaji nchini si wa kiwango cha kuridhisha. Hawamaanishi kile wanachokihubiri!

Hivi karibuni, niliweza kutembelea na kujionea juhudi na mchango wa shirika la ActionAid-Tanzania ambalo lilishirikiana na vikundi na AZAKI za Pemba mathalani taasisi ya wakulima wa karafuu (ZACPO) ambapo walisimamia kuhakikisha bei ya zao la karafuu inakuwa kwa maslahi ya wakulima na kumudu kuipandisha toka iliyokuwapo TZS 3,500/- kwa kilo moja hadi TZS 13,000/-. Ongezeko ambalo linakuwa faraja hasa kwa wakulima na kuwapa hata shime katika uzalishaji. Au kutetea bei ya mwani ambapo awali ilikuwa TZS 120/- kwa kilo moja hadi kufikia TZS 400/- kwa kilo moja.

Mifano kama hii ipo mingi; ingawa bado kwa upekee wa mchango wa AZAKI haitoshi. Mchango wa AZAKI mbalimbali zinadhihirisha inawezekana kuleta mabadiliko chanya na yenye tija kwa sekta ya kilimo na hasa kumkwamua mkulima hasa wakulima wadogo wadogo.

Ni ukweli taasisi za kiserikali kama SIDO na nyinginezo zimekuwa zikiendesha mafunzo na kuwajengea uwezo hasa wakulima kuhakikisha wanazalisha mazao na kuyaweka katika kiwango cha hali ya juu tayari kwa kutumika “fine products”. Lakini bado wafanyabiashara na wawekezaji hawajawekeza nguvu za kutosha kuhakikisha bidhaa za kufanikisha tunazalisha na kutengeneza mazao yetu katika hali ya kutumika “fine products” zinapatikana kwa urahisi na unafuu hasa vijijini. Kwani wakulima wengi wamekuwa na kilio cha muda mrefu cha ukosefu wa vifungashio na vifaa vingine ambavyo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha mazao yao yanaingia sokoni katika hali itakayowapa faida zaidi kuliko sasa.

Lazima tuseme inatosha! Tuseme wakati ni sasa kuhakikisha tunahakikisha kilimo chetu kinawakwamua hasa wakulima wadogo wadogo. Kila mwenye shibe ahakikishe anafikiri mbinu ya kuhakikisha mkulima anakwamuka katika hali duni aliyopo. Na kwa viongozi; kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu utekelezaji wa sera na mipango tulizojiwekea ili tupate matunda halisi tunayo yatamani.


HPV: Virusi hatari zaidi kwa wanawake!

$
0
0

HPV ni kifupi cha maneno Human Papilloma Virus. Virusi vya HPV ni kundi la virusi lenye aina zaidi ya 150 ya virusi vinavyohusiana.

Virusi hivi huvutiwa na ngozi na sehemu zenye unyevunyevu kama kwenye uke, mkundu, kichwa cha uume, mdomo, koo na mapafu. Virusi hivi hushindwa kusitawi kwenye sehemu nyingine za mwili.

HPV-viruses

mapumbu-hpv-affected

Ukweli ni kwamba, mamilioni ya wanawake ulimwenguni pote huambukizwa virusi hivyo ambavyo inasemekana ndio ugonjwa wa zinaa ambao huwapata watu wengi zaidi. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), virusi hivyo ndivyo kisababishi kikuu cha kansa ya mlango wa tumbo la uzazi. (Mlango wa tumbo la uzazi ni sehemu nyembamba iliyo katikati ya uke na tumbo la uzazi la mwanamke.)

Kila mwaka, mamia ya maelfu ya wanawake huchunguzwa na kupatikana na virusi vya HPV na kila mwaka maelfu hufa kwa sababu ya kansa ya mlango wa tumbo la uzazi ambayo husababishwa na virusi hivyo. Virusi hivyo ndivyo kisababishi kikuu cha kansa inayowaua wanawake wengi katika nchi maskini.

Ulimwenguni pote, kansa ya mlango wa tumbo la uzazi ndiyo aina ya pili ya kansa inayoathiri sehemu za tumbo la uzazi ambayo huwapata wanawake wengi. Haishangazi kwamba, shirika la WHO husema kwamba virusi vya HPV ni 'Tatizo kubwa la afya ulimwenguni pote.'

NI MAMBO GANI UNAYOPASWA KUJUA KUHUSU VIRUSI HIVYO?
Virusi vya HPV hufanya wanaume na wanawake wapatwe na vipele vigumu, kutia ndani vipele vinavyotokea kwenye viungo vya uzazi. Kwa kawaida, vipele hivyo havina kansa. Ingawa kuna aina za virusi vya HPV zaidi ya 100, ni chache sana kati yazo ambazo husababisha kansa. Mtu hupata kansa ya mlango wa tumbo la uzazi ikiwa tu aina fulani ya virusi hivyo vinakaa kwa muda mrefu. Kwa upande mwingine, maambukizo mengi ya virusi hivyo hupona yenyewe baada ya kushindwa nguvu na mfumo wa kunga wa mwili.

WANAOWEZA KUAMBUKIZWA:
Wale hasa wanaoweza kuambukizwa ni wanawake wanaoanza kufanya ngono wakiwa na umri mdogo, wale walio na wapenzi wengi wanaume, au wale wanaofanya ngono na mwanaume ambaye ana wapenzi wengi wanawake. Mara nyingi, mwanamume asiye na dalili zozote zinazoonekana za ugonjwa huo ndiye humwambukiza mwenzi wake.

Hata hivyo, katika nyakati fulani, wanawake walio safi kimaadili au wale ambao labda hawajawahi kufanya ngono huambukizwa virusi hivyo. Kwa mfano, uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha kwamba mtoto anaweza kuambukizwa virusi hivyo mama anapojifungua. Ugonjwa huu unaweza kujitokeza miaka mingi baada ya mtu kuambukizwa.

JINSI YA KUJUA IKIWA UMEAMBUKIZWA:

Dalili za ugonjwa huo hazijitokezi waziwazi. Hatua muhimu ni kufanyiwa uchunguzi wa chembe za mlango wa tumbo la uzazi, yaani Pap Smear, au Papanicolaou Smear. (Uchunguzi huo ulipewa jina la daktari Mgiriki, George N. Papanicolaou, ambaye alivumbua mbinu ya kutia chembe rangi ili kuzichunguza.)

Ili kufanya uchunguzi huo, daktari hutoa chembe chache za mlango wa tumbo la uzazi na kuzipeleka kwenye maabara ili zichunguzwe. Uchunguzi huo unaweza kuonyesha ikiwa mtu ameambukizwa, ana uvimbe, au ana chembe zisizo za kawaida. Inaripotiwa kwamba uchunguzi wa Pap Smear umepunguza idadi ya watu wanaopatwa na kansa ya mlango wa tumbo la uzazi na vifo vinavyosababishwa na kansa hiyo.

Ikiwa matokeo ya uchunguzi huo hayaridhishi, kifaa maalumu chenye kamera hutumiwa kuchunguza sehemu iliyoathiriwa. Kwa kutumia kifaa hicho, daktari anaweza kuona kama kuna kidonda au la. Sehemu za tishu zilizoathiriwa hukatwa na kufanyiwa uchunguzi, kisha matibabu huanza.

Siku hizi, uchunguzi wa hali ya juu sana unaweza kufanywa kwenye maabara. Uchunguzi huo unaweza kuonyesha vizuri zaidi ikiwa mtu ameambukizwa.

MATIBABU NA KINGA:
Kuna matibabu kadhaa yanayoweza kudhibiti maambukizo ya HPV. Wataalamu hutumia dawa za kupaka. Baadhi ya dawa hizo huharibu chembe zenye virusi hivyo, na wengine husaidia mfumo wa kinga kupambana na virusi hivyo. Matibabu mengine hutia ndani kuondoa sehemu iliyoathiriwa kwa kutumia umeme, leza, au kwa kuigandisha. Hata hivyo, badala ya kufanyiwa upasuaji, ingefaa mtu aepuke kuambukizwa.

MTU ANAWEZAJE KUEPUKA KUAMBUKIZWA?
Usifanye ngono kabla hujaolewa. Pia ili kuzuia kansa ya mlango wa tumbo la uzazi, ni lazima wenzi wawe waaminifu. Hata hivyo, ni muhimu kujua kuhusu HPV kwa kuwa unaweza kuzuia usiambukizwe virusi hivyo. Isitoshe, hata kama maambukizo hayo yanajitokeza na kuenea, bado unaweza kutibiwa.

Shirika la WHO linasema: 'Mara nyingi kansa ya mlango wa tumbo la uzazi inaweza kutibiwa ikigunduliwa mapema.'

Mbali na kujifunza kuhusu maadili, wanawake wanapaswa kujua kuhusu ugonjwa huo na kuelewa umuhimu wa kufanyiwa uchunguzi mbalimbali kwa ukawaida kama vile Pap Smear. Uchunguzi huo unapaswa kufanyiwa mtu anapofikia umri wa miaka 18 au anapoanza kufanya ngono. Kasoro yoyote ikigunduliwa, mwanamke anaweza kutibiwa.

Bado wanasayansi wanaendelea kutafuta njia rahisi na zenye matokeo zaidi za kuchunguza virusi vya HPV. Pia, chanjo za kuzuia na kutibu ugonjwa huo zinaendelea kutengenezwa.

Soko la China: Fursa iliyo wazi kwa watanzania, tunayoichezea!

$
0
0

Mwezi Julai 2012, serikali ya Tanzania ilituma ujumbe mkubwa wa kiutendaji hapa Beijing – China, uliokusanya watu kutoka Wizara, Idara, Makampuni, Jumuiya na Taasisi mbalimbali za Tanzania, ukiwa na lengo la kutafuta fursa za biashara kwa ajili ya Tanzania na watanzania.

Kwenye mkutano huo wa mawaziri wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), lengo kubwa lilikuwa viongozi wa kisiasa kuangalia maendeleo ya ushirikiano kati ya China na Afrika, na viongozi wengine watendaji walikuwa wakiangalia ni vipi wataweza kupata fursa zenyewe na kuzitumia. Kuna mambo mawili makubwa niliyoyaona, moja la kufurahisha na lingine la kusikitisha katika mkutano huo.

Nilifurahi sana kwakuwa toka nianze kufuatilia ushiriki wa Tanzania kwenye mikutano ya kimataifa, huu ndio ushiriki nilioushuhudia kwa macho yangu ukiwa ni ushiriki wa maana. Wajumbe waliokuja walionekana wazi kuja wakiwa na malengo halisi, na kupigania kufikia malengo hayo. Nakumbuka jinsi Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje Bw John Haule, alivyokuwa akiratibu wajumbe ili kuendana na malengo waliyojia, nakumbuka maofisa vijana kutoka Wizara ya Mambo ya Nje wakiongozwa na Bw Kairuki, na hata maofisa wa ubalozi walivyokuwa wakifanya kazi kubwa kuusaidia ujumbe wa Tanzania. Nikiwa mtanzania niliona fahari kubwa kuona maofisa wa ubalozi, wafanyabiashara, wakulima, wanasiasa wanafanya kazi kwa pamoja kwa lengo moja.

wachina-watanzania

Lakini jambo moja kubwa lililonisikitisha ni kwamba, kuna baadhi ya mambo ambayo ni ya muhimu sana, lakini wajumbe wengi walikuwa hawayajui. Jambo hilo ni kuwa watendaji kutoka kwenye maeneo ya uzalishaji wa mazao walikuwa hawajui kama mazao yao yanahitajika kwenye soko la China, na yanaweza kuingia kwenye soko la China bila kutozwa ushuru. Maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na maofisa wa ubalozi wanajua kuwa kuna orodha kubwa ya bidhaa kutoka Tanzania zinazoweza kuingia kwenye soko la China bila kutozwa ushuru, na habari hizo wanazifikisha kwa jumuiya za wakulima na wafanyabiashara. Pamoja na hilo inasikitisha kwa kuwa kila kukicha kuna kilio cha wakulima wa Tanzania kuhusu masoko ya mazao yao. Nakumbuka niliongea na Profesa Haji Semboja aliyeiwakilisha bodi ya korosho, alinieleza kwa masikitiko jinsi mkulima wa korosho wa Tanzania anavyoibiwa na wafanyabiashara wanaonunua korosho moja kwa moja kutoka kwa wachuuzi kwa bei ya chini sana, wakati wangeweza kuuza korosho hiyo kwa bei nzuri sana kwa wanunuzi wa China.

Sababu kubwa kwanza ni kuwa hakuna mipango na nguvu ya pamoja ya kutumia soko la China. Soko la China ni kama kinywa kikubwa kinachohitaji chakula kingi, ambacho wakulima wadogo wadogo wakiwa mmoja mmoja hawawezi kukidhi mahitaji yake. Bila kuwa na uzalishaji wa maana, kwa maana ya kiasi na ubora, bado tutaendelea kuliangalia soko la China bila kunufaika nalo vya kutosha. Ili kutumia soko la China, kunahitajika kuwe na uzalishaji mkubwa na wa muda mrefu, na si ule wa kulima leo, kuuza kesho na kufurahia mapato kidogo na kuacha uzalishaji na kusahau soko. Wachina huwa hawafanyi biashara kwa mtindo huu, wanapenda mshirika wa biashara mwenye uwezo wa kutoa bidhaa nyingi na kwa muda mrefu. Na kibaya zaidi ni kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao wameona udhaifu huu, na kuamua kununua bidhaa kwa wakulima wadogo wadogo na kuweka hali fulani kama ya “kuhodhi” soko, na kumpunja mchuuzi.

Mwishoni mwa mwezi Agosti, China ilitoa waraka kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika, ukiendelea maendeleo changamoto na mustakbali wa uhusiano wa uchumi na kibiashara kati ya China na Afrika. Waraka huo umezungumzia mambo mengi, ikiwa ni pamoja na ongezeko la kasi la biashara kati ya China na Afrika, ongezeko la uwekezaji wa China barani Afrika na maeneo uwekezaji huo unakoelezwa, na hata changamoto zilizopo kwenye ushirikiano huo.

xin-kikwete

Kwa watu tunaofuatilia mambo yanayohusu uhusiano kati ya China na Afrika, na China na Tanzania waraka huu si jambo jipya sana kwa sababu yaliyomo ni yale ambayo tayari yamekuwa yakifanyika na yanaendelea kufanyika. Isipokuwa waraka huu ni majumuisho na maelezo ya mambo yaliyofanyika tangu China itoe msukumo mpya kwenye uhusiano kati yake na nchi za Afrika, hasa tangu baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) lilipoanzishwa mwaka 2000. Lakini vilevile waraka huu unaonesha ni jinsi China ilivyojipanga vizuri katika kuendesha uhusiano na ushirikiano kati yake na nchi za Afrika.

Pamoja na kuwa lengo la uwekezaji na biashara ni kupata faida, kwenye waraka huo pia tunaweza kuona kuwa China haina nia ya kujinufaisha tu, bali pia ina udhati wa kuzisaidia nchi za Afrika, kama zikijipanga vizuri na kama zikiwa na nia ya dhati ya kutaka kujiendeleza. Aya tano za waraka huo (kuhimiza maendeleo endelevu ya biashara, kuboresha uwekezaji na ushirikiano kwenye mambo ya fedha, kuhimiza ushirikiano kwenye shughuli za kilimo na usalama wa chakula, kuunga mkono ujenzi wa miundo mbinu, kuboresha maisha wa watu na kuwajengea uwezo wa kujiendeleza, pamoja na kuhimiza ushirikiano kati ya nchi mbalimbali za Afrika), zote zinaonesha udhati wa China katika kushirikiana na watu wa Afrika katika kuleta maendeleo. Lakini tukijiangalia sisi wenyewe waafrika, au tukijiangalia sisi watanzania tunaweza kuona kuwa bado kuna kitu kinapungua kwenye ushirikiano wetu wa kibiashara na marafiki zetu. Ni kama tunakosa udhati kwenye kufanya biashara, hata pale tunapopewa fursa ya soko kubwa kama la China kwa mashariki nafuu, tunashindwa kuwatangazia wakulima wetu kuwa sasa tunatakiwa kujipanga tulime kwa wingi mteja yuko tayari.

China inajua kuwa sehemu kubwa ya watu wa nchi nyingi za Afrika, kama ilivyokuwa China katika miaka michache iliyopita, ni wakulima. Kama nguvu kazi nyingi ya watu katika nchi iko kwenye kilimo, basi kuwa makini na kilimo na wakulima, kuna matokeo mazuri kwa watu hao na nchi kwa ujumla. Ni kutokana na kuelewa ukweli huo, na ni kutokana na uzoefu wake, ndio maana China ikaona kuwa, pamoja na kuendelea kuwapatia misaada mingine, ni vizuri kuwasaidia marafiki kwa kuwawezesha katika maeneo mbalimbali, na hata kuwapatia soko la bidhaa na mazao yao.

Lakini kwa sisi watanzania tukijaribu kujiangalia kwa undani, tunaweza kuona baadhi ya mambo tunayofanya katika ushirikiano kati yetu na China yanatakiwa kuboreshwa. Kwa mfano, unapozungumzia kuhusu kutumia fursa ya soko la China kwa bidhaa za kilimo tunazozalisha Tanzania, utaona kuwa kuna kitu fulani kama kutupiana mpira. Maofisa wa serikali wanasema jukumu la serikali ni kuweka mazingira kwa ajili ya wakulima na wafanyabiashara kuchangamkia fursa hizo, serikali haiwezi kujiingiza huko. Ukiwauliza wakulima na wazalishaji wenyewe wanasema wanahitaji msaada ili waweze kunufaika na soko hilo, kwani wao kama wao bila mkono wa serikali, ni vigumu sana kunufaika na soko la China.

Ukichambua wanachoongea maofisa wa serikali, utaona ni sawa na kile tunachokisikia wanachoongea wanasiasa wa Marekani, au nadharia za uchumi za uchumi za mwanafalsafa Adam Smith, kuwa serikali hazipaswi kujiingiza kwenye mambo ya uzalishaji na biashara, kwa kuwa haya ni majukumu ya watu si majukumu wa serikali. Lakini tunatakiwa kukumbuka kuwa Marekani na Tanzania zina mazingira tofauti sana, wamarekani wana uwezo mkubwa wa kufanya shughuli za uzalishaji na kwenda kuziuza katika masoko ya sehemu mbalimbali duniani. Tena wao hawapendi serikali iwaingilie, isipokuwa wanataka serikali ifanye kazi ya kuweka mazingira ya kuwawezesha kufanya shughuli zao.

Lakini Tanzania si Marekani. Tukiangalia ukweli wa mambo kuhusu uwezo wa wakulima wetu na wafanyabiashara kufanya biashara ya kimataifa ni mdogo sana, hauwafikii hata ule wa baadhi ya majirani zetu, bila msaada madhubuti wa serikali, hawawezi kwenda popote, baadhi hata wanashindwa kufanya biashara ndani ya Tanzania. Mfano mmoja nilioushuhudia kwenye maonesho ya biashara hapa China ni kuwa, kuna mnunuzi mmoja alipenda sanaa za kazi za mikono, na alisema zinafaa sana kwa biashara zake, lakini alipopewa oda ya makontena kumi kwa mwaka alisema anaweza kujitahidi kutoa robo kontena kwa mwaka. Huyu ni mfanyabiashara aliyekuja China kutangaza bidhaa zake kwa juhudi zake binafsi, kama angewezeshwa, huenda watanzania wengi zaidi wangenufaika na fursa yake.

Tukiangalia China inavyojipanga katika kushirikiana na nchi za Afrika na hata Tanzania, unaona kabisa kuwa serikali ya China haijiweki pembeni kuwasaidia wafanyabiashara wanaotaka kuwekeza na kufanya biashara Afrika. Kwa mfano kuna Mfuko wa Maendeleo kati ya China na Afrika (CAD Fund), mfuko huu unalenga kuwasaidia wafanyabiashara wa China wanaotaka kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo katika nchi za Afrika, hasa miradi inayozinufaisha pande zote mbili. Mfuko huu unataja wazi ni maeneo gani ambayo yanapewa kipaumbele, na hata namna ya kuwasaidia wachina wanaotaka kufanya biashara katika nchi za Afrika.

Lakini tukiangalia upande wetu wa Tanzania, ni vigumu kuona mpango ulio wazi wa kutumia na kunufaika na soko la China. Serikali bado haina mfuko wowote unaofanana na CAD Fund, japo kusaidia wafanyabiashara wa Tanzania kuuza bidhaa zao China, au hata utaratibu unaotaja ni bidhaa gani ambazo inaweza kutoa msukumo na kuhimiza uzalishaji wake, kuwahamasisha na kuwasaidia watu kuzalisha bidhaa hizo ili tutumie soko la China. Serikali inaweka mkazo kwenye sera za jumla (macro policies), lakini kuwa na sera peke yake bila hatua za kuisukuma sera hiyo, hatuwezi kuwa na matokeo yoyote ya maana. Wakulima na wafanyabiashara hawafahamishwi wazi kuhusu fursa zilizopo, na wachache wanaofahamu hawasaidiwi kunufaika na fursa hizo. Matokeo yake ni kuwa fursa ipo, tunaiongelea tu bila kuitumia.

Kama serikali yetu ingekuwa na sera ya wazi, inayosema tutauza kahawa, korosho au tumbaku kwa wingi, basi ni bora ingewahimiza wakulima wa mazao hayo, kuwapa msaada wa fedha, kiufundi na kiutalaamu na kusimamia kwa nguvu uzalishaji mkubwa wa mazao hayo, na kwenda kutumia soko la China. Ni vigumu sana kwa mzalishaji mmoja mmoja peke yake bila kupata msaada madhubuti kutoka kwa serikali kuweza kutumia fursa hiyo. Vinginevyo tutaendelea kuongea na kufurahia kuhusu kuwepo kwa fursa hiyo, bila kunufaika nayo hata kidogo.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, kuna orodha ya zaidi ya bidhaa 4,700 kutoka kwa nchi za Afrika zenye uhusiano wa kibalozi na China, zinazoweza kuingia kwenye soko la China bila ushuru. Idadi hii ya bidhaa si ndogo, na huenda unahusu mazao yote tunayozalisha katika eneo lote la Tanzania. Kama watanzania (serikali, wakulima na wafanyabiashara) tukijipanga, na kutumia vizuri fursa hii. Kuna uwezekano mkubwa sana wa kupiga hatua katika kuwaendeleza wakulima na wafanyabiashara. Lakini kama mtu mmoja mmoja akiachwa atumie fursa hii, mchakato mgumu na mrefu unaweza kufanya tushindwe kunufaika nayo.

Kilichopo kwa sasa ni kuwa, kwenye upande wa siasa uhusiano ni mzuri sana, urafiki kati ya China na Tanzania upo kwenye kiwango cha juu sana. Wenzetu wachina wamejipanga vizuri na kunufaika na ushirikiano huo. Kama watanzania tutaendelea kuona fahari ya urafiki tu, bila kutumia fursa ya urafiki mzuri iwe fursa ya biashara, basi tutakuwa tunachezea fursa iliyopo.

nyerere-mao

Rais wa China na mwenyekiti wa CPC Mao Zedong akisalimiana na Mwenyekiti wa Tanganyika African National Union (TANU) na Rais wa Tanzania J.K.Nyerere – Machi 25, 1974

Tuimarishe sheria na sera zetu, tukusanye kodi!

$
0
0

Hivi karibuni tunashuhudia duniani nchi mbalimbali zikihaha kuhakikisha suala la kodi linakuwa la kipaumbele. Kuhakikisha nchi zinapata kodi stahiki toka kwa vyanzo vyote hususan vile vya ndani. Suala hili kwa uzito wake limekuwa miongoni mwa ajenda kuu katika mikutano mbalimbali ya kimataifa mathalani ule wa G20 wa hivi karibuni. Kwanini sasa?

Suala hili, kwa nchi zinazoendelea zenye kuendesha serikali zao kwa kutegemea kiasi kikubwa misaada toka nje ya nchi zao ni la muhimu sana. Kwani, kiasi kikubwa sana kimekuwa kikipotea katika mianya mbalimbali ya ukwepaji kodi huku nchi hizo zikiendelea kutumia muda mwingi na rasilimali katika kusaka misaada.

Hayati Mwalimu Julius Nyerere, mnamo Machi 13, 1995 katika hotuba yake maarufu ambayo aligusia “nyufa” zenye kuangamiza taifa endapo zisiposhughulikiwa ilikuwa pia suala la kutokukusanya kodi.

Mwalimu, alienda hatua kadhaa mbele kuweza kuonyesha na kudhihirisha uhusiano wa karibu sana kati kutokukusanya kodi na rushwa.

“Serikali corrupt haikusanyi kodi. Itabaki kufukuzana fukuzana na vijitu vidogo vidogo mabarabarani hivi basi” - Mwalimu Julius Nyerere.

Kwa kiasi kikubwa yale ambayo Mwalimu alikuwa akitahadharisha juu ya kuacha kukusanya kodi na hasa kukusanya kodi kwa wote yaani wananchi na taasisi zote na sio kuweka msukumo upande mmoja, kwa wananchi wadogo wadogo bado mpaka sasa hali inaendelea. “Sikio la kufa halisikii dawa” wahenga walipata kunena.

Tunaona juhudi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kuhakikisha kodi inakusanywa. Kubuni njia mbalimbali mathalani matumizi ya vifaa vya kieletroniki vya EFD, na malipo mengine kama ya kulipia ushuru wa magari kwa kupitia mitandao. Juhudi ambazo si za kubezwa. Lakini bado haiondoi fursa ya kuhoji kwa mapana; hasa juu ya ukusanywaji wa kodi stahiki toka kwa vyanzo vya mapato vikubwa kama makampuni makubwa ya kimataifa na wafanyabiashara wakubwa.

Kwa haraka haraka; bado TRA inajihusisha sana na kutumia nguvu nyingi kwa vile “vijitu vidogo vidogo” ambavyo Mwalimu Nyerere alikuwa akivigusia huku makampuni makubwa na wafanyabiashara wakineemeka kutokana na mazingira duni ambayo tumejiwekea wenyewe kupitia sheria na sera mbalimbali zenye kutoa misamaha mikubwa ya kodi achilia mbali uwezo wa makampuni hayo kutumia wataalamu katika kukwepa kulipa kodi.

Mazingira ya kisera  ambayo tunapaswa kuzingatia ni pamoja na kuhakikisha ulipwaji wa kodi unakuwa wa haki kwa kila raia. Tajiri maarufu duniani, Warren Buffet alipata kukiri kupitia vyombo vya habari kuwa sekretari wake, Debbie Bosanek alikuwa analipa kodi kiwango kikubwa sana kuzidi hata ambacho yeye analipa.  Bosanek alikuwa akilipa kodi ya kiwango cha asilimia 35.8 cha kipato chake huku bilionea Buffet alikuwa akilipa asilimia 17.4 tu!

Hali hiyo iliweza kutokea tu kutokana na mfumo wa kisera wa kodi uliopo nchini Marekani. Jambo ambalo liliushtua ulimwengu na hasa wanaharakati wanaopigania haki katika masuala ya kodi.

Tukumbuke hayo yaliweza kutokea katika nchi kama Marekani yenye mifumo imara ya kuhakiki, kufatilia kodi na kukusanya kodi; je hali ipoje kwa nchi kama yetu Tanzania ambapo tunamifumo dhaifu mingi katika kufatilia na kuhakiki ulipwaji kodi? Ni matajiri wangapi kwa utashi na makusudi wanakwepa kodi huku walalahoi wakizidi kubanwa kwa kodi kadha wa kadha.

Baya moja alihalalishi baya jingine, hivyo si lengo la uchambuzi huu wa makala kuwahamasisha wananchi wa kipato cha chini kutolipa kodi; bali hasa kuzisukuma mamlaka husika na watendaji kusimamia vyema haki katika kutoza kodi stahiki kwa kila raia, taasisi, makampuni na wazalishaji.

Uwepo wa sheria zenye kutoa mianya kutumiwa vibaya na wawekezaji hususan wa nje na makampuni makubwa ni pamoja na; sheria ya ukanda wa uzalishaji kwa ajili ya kusafirisha (Export Processing Zone Act, 2002), Sheria ya mwaka 1997 ya Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Act, 1997) na Ukanda maalumu wa uzalishaji ya mwaka 2005 (Special Economic Zone, 2005).

Katika sheria hizo tunaweza kuna misamaha ya ulipaji wa kodi kwa miaka kumi. Lakini pia misamaha katika bidhaa (capital goods and raw materials) ambapo huko nako kuna kunaweza kutumika kuepa kodi inayopaswa kulipwa.

Tukiangalia sheria nyingine ya kodi ya mapato kwa makampuni; “corporate income tax” ambapo kwa Tanzania makampuni yananeemeka nafuu ya punguzo la kodi kwa asilimia 25. Hii ni tofauti hata kwa nchi nyingine za kiafrika katika sheria hiyo hiyo. Tukichukua mfano: Nigeria ambapo kwa sheria hiyo hiyo wao wanatoza nafuu ya kodi kwa asilimia 30, Ghana kwa asilimia35 au Afrika Kusini kwa asilimia 28!

Kisingizio kikubwa kikiwa ni kuvutia uwekezaji na kutoa fursa ya ajira na uzalishaji; jambo ambalo linapingwa na wataalamu wa kiuchumi kuwa kiwango cha misamaha hakiendani na namna ambavyo taifa linaneemeka kwa kodi.

Eneo hili la misamaha ya kodi ni eneo ambalo kwa miaka mingi sasa limekuwa likiandikwa na kulalamikiwa na Mkaguzi mkuu na mdhibiti wa hesabu za serikali (CAG); hii ikiwa ni pia kutoa ushauri wa kuwekwa ukomo kisera na kisheria katika kiwango cha kutoa misamaha hiyo. Kwa mwaka 2011 CAG alishauri serikali iweke aidha ukomo wa utoaji wa misamaha ya kodi isiyozidi asilimia 5 ya jumla ya mapato yaliyokusanywa au kuacha kabisa kutoa misamaha hiyo ya kodi kwa makampuni na watu ambao kiuhalisia wanaouwezo kabisa wa kulipa kodi.

Na ifahamike, wanaoneemeka sana na misamaha hii ni makampuni makubwa na si mashirika ya kidini kama ambavyo miaka michache iliyoaminishwa kama njia ya propaganda kuendelea kutetea uwepo wa misamaha.

Uchambuzi wa shirika la Uwazi uliotolewa mwaka 2010 na kupewa jina; “Misamaha ya Kodi Tanzania: Ipo juu sana na kutufanya kwa kiasi kikubwa kutegemea misaada ya nje” ulibainisha misamaha ya kodi iliyotolewa katika mwaka wa kibajeti wa 2008/09-2009/10 makampuni ya madini yalipata misamaha takribani asilimia 7.51 huku makampuni binafsi na watu binafsi wakipewa misahama ya asimilia 6.00. Na vinara wa kuneemeka na misamaha ya kodi wakiwa ni wale wenye vyeti vya uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Ukuzaji wa Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) ambapo inafikia asilimia 45. Asilimia kubwa ya makampuni yenye vyeti/hati hizo ni makampuni ya kimataifa.

Taasisi za kidini kwa uchambuzi wa bajeti kwa mwaka huo zilikuwa zinapata kwa asilimia 0.05 tu huku mashirika yasiyo ya kiserikali yakiwa yanapata asilimia 4.06! Huo ndiyo ukweli. Huo ndio uhalisia.

Uhalisia wa mianya iliyopo na mbinu zinazotumika na makampuni hasa ya kimataifa ni nyingi sana ambazo zinapaswa kuendelea kuanikwa kwa makala zijazo kwa manufaa hasa ya wananchi kufahamu uhalisia wapi mianya ya upotevu wa fedha inakuwapo ambapo serikali inashindwa kutumia fursa hizo ili kuhakikisha inapata fedha za kuzitumia katika kutoa huduma bora za kijamii kama elimu, afya, maji safi na salama.

Ni wakati sasa wa kusema inatosha na kuamua kuziboresha sera na sheria zetu za Tanzania na kuhakikisha zinatoa fursa madhubuti za kukusanya kodi na kuondosha mianya yote ya ukwepaji kodi. Tunao uwezo kabisa wa kuboresha makusanyo ya kodi na kumudu kutekeleza mikakati mbalimbali ya kimaendeleo kwa fedha zetu wenyewe stahiki endapo tutatumia vyema wataalamu wetu na kuhakikisha sera, sheria na mifumo inakuwa imara kudhibiti ukwepaji wowote unaoweza kutokea.

Saratani ya Matiti (Breast Cancer): Chanzo, Dalili na Matibabu yake

$
0
0

Kansa ya matiti ni aina ya kansa inayojitokeza toka tishu za matiti hasa mirija myembamba inayopitisha maziwa. Ugonjwa huu (Saratani ya matiti) hutokea kwa binadamu na mamalia wengine. Idadi ya wanaume wanaopatwa na kansa ya matiti ni ndogo sana ikilinganishwa na ya wanawake.

Ulimwenguni pote, kansa ya matiti hubeba asilimia 29 nukta tisa ya kansa zote kwa wanawake.

Licha ya maendeleo ya kitiba, bado kansa ya matiti ndiyo kansa inayosababisha vifo vingi zaidi vya wanawake.

Nchi zilizoendelea za Amerika Kaskazini na Ulaya Magharibi ndizo zenye idadi kubwa zaidi ya watu walio na kansa, lakini idadi ya wanawake walio na kansa ya matiti inaongezeka katika bara la Asia na Afrika ambako kwa kawaida kumekuwa na idadi ndogo kiukweli.

Idadi ya wanaokufa kati ya wale wanaogundulika kuwa na ugonjwa huo huko Asia na Afrika ni ya juu kwasababu kansa hiyo haigunduliwi mapema. Wagonjwa wengi huja ikiwa tayari imeenea sana.

Kansa ya matiti huanza wakati ambapo chembe moja inajigawanya haraka sana isivyo kawaida na bila utaratibu, na hatua kwa hatua inafanyiza uvimbe.

Uvimbe unakuwa kansa wakati chembe zake zinapovamia tishu nyingine. Uvimbe fulani unaweza kuchukua miaka kumi hivi kabla ya kugunduliwa.

VIHATARISHI/VISABABISHI

Hatari ya kupatwa na kansa hiyo huongezeka dadiri umri unavyosonga. Asilimia 80 hivi ya wanawake wenye kansa ya matiti wana umri unaozidi miaka 50.

Lakini jambo linalofariji ni kwamba kansa ya matiti ni mojawapo ya kansa zinazoweza kutibiwa kwa urahisi.

Watakao tibiwa kabla ya kansa hiyo kuenea wanaweza kuishi muda mrefu kwa ukawaida.

Visababishi vya kansa ya matiti bado ni fumbo.

Baadhi ya wanasayansi wanaamini kwamba kansa ya matiti hutokana na hatua nyingi tata ambazo huanza wakati ambapo chembe fulani ya urithi yenye kasoro inapofanya chembe zitende kwa njia isiyo ya kawaida, yaani, zigawanyike kwa kasi sana, zishambulie tishu nyingine na kuepuka kuharibiwa na mfumo wa kinga, kisha pole pole chembe hizo zinashambulia na kuharibu viungo muhimu vya mwili.

Jambo lingine linalohusishwa na kansa ya matiti ni homoni ya estrojeni ambayo huenda inachochea aina fulani za kansa hiyo.

Kwa hiyo, mwanamke anaweza kupatwa na kansa hiyo ikiwa alianza kupata hedhi mapema maishani au ikiwa aliacha kupata hedhi akiwa amechelewa isivyo kawaida, ikiwa alipata mimba ya kwanza umri wake ukiwa umesonga au ikiwa hakuwahi kupata mimba, au ikiwa alipata matibabu ya kurudisha homoni fulani mwilini.

Kwa kuwa chembe za mafuta hutokeza estrojeni, huenda wanawake walionenepa kupita kiasi waliofika umri wa kuacha kupata hedhi na hivyo ovari zao hazitokezi tena homoni, wakawa katika hatari ya kupatwa na kansa hiyo.

Pia watu walio na viwango vya juu vya insulini na watu walio na viwango vya chini vya homoni ya usingizi inayoitwa melatonia kama vile watu wanaofanya kazi usiku, wako pia katika hatari ya kupatwa na kansa hiyo.

Uvutaji wa tumbaku umeonekana kuongeza hatari zaidi ya kupata saratani ya matiti, kiwango kikubwa cha tumbaku iliyovutwa na kuanza kuvuta tumbaku katika umri mdogo hufanya hatari kuongezeka zaidi.

Mionzi na kemikali za viwandani huongeza hatari ya kansa ya matiti. Kemikali kama polychlorinated biphenyls, polycyclic aromatic hydrocarbons na dawa za kuulia wadudu huchangia kutokea saratani hiyo.

DALILI

- Uvimbe wowote au kuongezeka kwa unene wa ngozi kwenye makwapa au titi.

- Umajimaji wowote unaotoka kwenye chuchu ambao si maziwa.

- Mabadiriko yoyote ya rangi au ngozi ya titi.

- Chuchu iliyodidimia kwa njia isiyo ya kawaida au inayowasha.

UCHUNGUZI KUJUA KAMA NI KANSA

Ili kuchunguza ikiwa uvimbe una kansa sindano nyembamba hutumiwa kutoa tishu kutoka kwenye uvimbe huo na kufanyiwa uchunguzi.

MATIBABU

Uvimbe ukiwa na kansa hufanyiwa upasuaji ili kuondoa uvimbe huo na tishu zinazozunguka titi. Upasuaji husaidia kuonyesha uvimbe ulipofikia (ukubwa, aina na kuenea kwake) na kuchunguza uvimbe unakua upesi kadiri gani.

Chembe zenye kansa zinaweza kutoka kwenye uvimbe na kusafiri kupitia mfumo wa damu au mfumo wa limfu na kuanza kukua tena mahali pengine mwilini.

Kuenea kwa kansa hadi kwenye viungo na tishu muhimu kama vile ubongo, ini, uboho wa mfupa au mapafu ndio hufanya ugonjwa huo uwe hatari.

Hivyo baada ya upasuaji, wagonjwa wengi hupata matibabu mengine ambayo yatazuia kansa isirudi na kuenea.

Kwasababu ya maendeleo katika matibabu ya kansa ya matiti, kumekuwa na matibabu mbalimbali ikitegemea umri, afya historia ya kansa katika familia, na aina ya kansa.

Wanasayansi wanajifunza mambo mengine kuhusu kansa kutia ndani kuelewa ni kwa nini kansa huenea, kudhibiti chembe za kansa ambazo haziharibiwi kupitia matibabu ya kemikali, kuzuia kugawanyika kwa chembe na kutibu kila uvimbe kwa njia hususa.

Ndoto ya China ni hii, ya Tanzania ni ipi?

$
0
0

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mjadala kuhusu wazo la fikra jumuiya (collective thinking) na mchango wake katika kuhimiza umoja, usalama na maendeleo ya nchi. Wazo hili limezua mjadala kwa kuwa kuna baadhi ya watu wanaona kuwa nchi yetu inapungukiwa kitu fulani, kwa hiyo inatakiwa kuwa na kitu hicho ili tujue tunaelekea wapi. Baadhi wanaona wazo hili si jambo halisi, linaongeleka tu lakini haliwezi kutekelezwa, kwa kuwa wanaona si rahisi kwa kundi kubwa la watu kufikiri kwa njia moja au kuwa na ndoto moja. Lakini wengine wanaona kuwa wazo hili ni jambo halisi na ni msingi wa mwongozo wa maendeleo ya nchi.

Ili kujua kama kweli wazo hili ni jambo la kufikirika tu au ni jambo halisi, ni vizuri tukijaribu kuziangalia nchi kwa kutumia mfano wa binadamu. Kwa kawaida kwa mtu anayeishi kwa kuangalia mbali, kujiwekea malengo na mipango ya kufikia malengo hayo, huwa ana mafanikio katika maisha yake. Lakini mtu anayeishi kwa mtindo wa kuzingatia mambo ya leo tu, na kukabiliana na changamoto za leo za kesho anamwachia Mungu, mara nyingi maisha yake yanakosa mwelekeo, leo anaweza kuwa na neema kubwa na kesho akawa na taabu kubwa, na mara nyingi mwisho wake unakuwa mbaya. Wachina wana methali moja inayosema usipoangalia mbali, taabu inakukaribia.

Kuna wakati nchi huwa zinakuwa na tabia kama za binadamu, zinafikiria, kupanga na kutekeleza mipango yake. Lakini kama ilivyo kwa binadamu, kuna baadhi ya nchi zinaonekana wazi kabisa kuwa na ndoto, na zinaonekana wazi kabisa jinsi zinavyofanya kazi kutimiza ya ndoto hizo. Nchi za namna hiyo kimsingi zinakuwa imara na zinapiga hatua. Lakini kuna nchi nyingine hazionekani kama zina ndoto au kuwa na mipango yoyote halisi ya kuendeleza nchi, au hata kufikiri nchi hiyo itakuwa na sura gani katika miaka 20 au hata 50 ijayo, ni kama zinaishi na kusibiri jua lichomoze na kuzama. Hazina ndoto ya kutaka siku moja ziwe nchi za namna gani. Nchi kama hizo hazitabiriki, kuna wakati zinakumbwa na majanga yasiyofikirika, na hata kuleta matatizo makubwa kwa nchi au jumuiya nyingine.

Kabla ya kujiangalia sisi watanzania tuko wapi, ni vizuri tuangalie nchi zilizojitangaza wazi kuwa zina ndoto ziko wapi na zinafanya nini katika kutimiza ndoto hizo. Katika siku za hivi karibuni China imekuwa ikitangaza kuhusu “ndoto ya China”. Kimsingi ndoto ya China inahusu nia ya wachina ya kuona nchi yao inakuwa na neema, na neema hiyo itatokana na wachina wenyewe kufanya juhudi kwa pamoja, kwa kufuata ujamaa unaolingana na hali halisi ya China. Kama nchi ikiwa na neema na ustawi, watu wake wanakuwa na neema. Ukiangalia maendeleo ya uchumi na jamii ya China kwa sasa, unaweza kuona wazi kabisa kuwa wachina wanafanya kazi, na wanaelekea kutimiza ndoto yao. Ukijaribu kuchambua kwa undani ndoto hii, kwa ufupi unaweza kuona kuwa inaeleza ni nini wachina kwa ujumla wao wanafikiri na kukifanya kwa ajili ya kuendeleza nchi yao.

Wamarekani pia wana ndoto yao American dream, wao wanaona kuwa nchi yao itakuwa na neema na nguvu kama watu wanaoishi katika nchi yao, bila kujali wanatoka wapi, wanaonekana vipi au wana imani gani, wanakuwa na fursa ya kuwa na neema na mafanikio. Kwa hiyo wamejitahidi kuweka mazingira ya haki ambayo mtu yoyote akifanya juhudi basi atakuwa na neema na mafanikio anayostahili. Na kama watu wakiwa na neema na mafanikio basi nchi yao pia itakuwa na neema na mafanikio.

Wazo la ndoto ya nchi ni suala la fikra jumuiya (collective thinking) Wazo hili linaweza kuonekana kuwa ni wazo la kufikirika tu (utopian) kwa kuwa labda watu wengi wenye hali tofauti, kama vile viwango vya elimu, mawazo, mazingira ya kuishi na upeo wao, hawawezi kufikiri kwa njia moja. Lakini tukiangalia hali halisi katika nchi ambazo zimetamka wazi kuhusu jambo hili na kulifanyia kazi, wazo hili linaonekana wazi kuwa ni kitu halisi, na linaweza kutekelezeka.  

Sisi watanzania kwa ujumla wetu tunatakiwa kujiuliza na kujua, ndoto yetu ni ipi? Tunataka kuipeleka wapi Tanzania? na vipi tunaipeleka Tanzania tunakotaka iende? Kwa sasa ni vigumu sana kupata majibu ya maswali haya. Wakati wa enzi za awamu ya kwanza tulikuwa na kitu kinachofanana na “ndoto ya Tanzania”, yaani kuijenga Tanzania kuwa nchi “ujamaa na kujitegemea”, ambayo wananchi wake wanaishi kwa haki, usawa na neema. Pamoja na kuwa ndoto hiyo ambayo ilitangazwa kuwa sera ya nchi ilikuwa inapingwa, ilieleza vizuri maana ya ujamaa na kujitegemea na kueleza wazi nini kinafanyika ili kujenga nchi ya ujamaa inayojitegemea, na hayo yalikuwa yanaonekana.

Mwaka 1992 tulipoanza kutekeleza mageuzi ya kimuundo (structural adjustment programmes), tuliyotakiwa kuyatekeleza na Shirika la fedha la Kimataifa IMF, ilionekana wazi kabisa kuwa ndoto yetu ilifutika. Tatizo ni kwamba baada ya kuondoa sera ya ujamaa na kujitegemea, hatukuleta kitu mbadala ambacho kinaeleza wazi kuwa tunajenga nchi ya namna gani. Mpango wa maendeleo ya Tanzania kuelekea mwaka 2025 (Vision 2025) uliotangazwa kama mbadala wa sera hiyo, ni dira tu inayotuongoza kwenda mwaka 2025, inaishia hapo tu haielezi Tanzania itaenda wapi baada ya hapo, lakini Tanzania na watanzania wataendelea kuwepo hata baada ya hapo.

Mwanataaluma mmoja wa Tanzania Dr Malima Bundala aliandika kitabu kinachotoa changamoto kubwa kwa watanzania kuhusu fikra jumuiya. Dr Bundala anaona kuwa jamii bila kuwa na fikra jumuiya, ni vigumu sana kwa jumuiya hiyo kupata maendeleo, au kuwa mwelekeo unaoeleweka. Kwa sasa sisi watanzania tunaonekana kuwa na udhaifu kwenye jambo hilo. Japo kuwa tunajidai na kujitangaza kuwa sisi ni watanzania, kimsingi tunaonekana kuwa tumeisahau kabisa Tanzania yenyewe. Inawezekana kuwa leo ukimuuliza mwanaCCM atakwambia “ndoto yangu ni kuona chama changu kinaendelea kutawala”, ukimuuliza mtu wa upinzani jibu litakuwa ndoto yangu kubwa ni kuiondoa CCM madarakani. Tunayojali zaidi ni mambo binafsi na jumuiya zetu ndogo ndogo, Tanzania tumeiweka mwisho kabisa.

Wakati umefika tukumbushane kuwa sisi ni watanzania na tunahitaji ndoto ya namna moja ya kitanzania, ambayo inaweza kutukumbusha tulikotoka, tulipo na tunakotaka kuelekea. Kana tukiendelea na mtindo wa kutoangalia mbali, basi mbeleni tuna hatari kubwa.

Viewing all 186 articles
Browse latest View live