Ni miaka mingi sasa tumekuwa tunaisifu China kuwa ni nchi iliyopiga hatua kubwa kimaendeleo, na mara kwa mara wanasiasa wetu wamekuwa wakiitaja China kuwa ni nchi ya mfano wa kuigwa, hasa kutokana na yale wanayosikia kutoka kwenye vyombo vya habari na yale wanayoyaona wanapofanya ziara zao nchini China.
Ukiwa unaishi nchini China kwenyewe, ni kweli unaweza kuona kuwa neno ‘maendeleo’ ni neno lenye maana hiyo, na si neno la kufikirika tu ambalo linatoka kwenye vinywa vya wanasiasa, hasa wale wanaopenda kutumia neno hilo kama njia ya kujionesha kuwa wana nia ya kuleta maendeleo. Ukiwa nchini China (nilipo, na nimekaa kwa takribani miaka kumi sasa), kila baada ya muda fulani unaweza kuona kuna kupiga hatua kwenye maisha ya watu wa kawaida, na hata ukiwauliza watu wa kawaida, wa mjini au vijijini, wa sehemu za mashariki zilizoendelea kiuchumi na sehemu za magharibi zilizoko nyuma kiuchumi, wote wanaweza kukwambia wanaweza kuona kuwa nchi yao inapiga hatua.
Mwanzoni nilikuwa nafurahi sana nilipokuwa naona viongozi wetu wanafanya ziara nchini China, kwa matarajio kuwa wanaweza kuona na kujifunza kinachofanyika hapa China, na kukitumia kule nyumbani.
Siwezi kuweka orodha ya mawaziri na maofisa wa serikali waliofanya ziara China, wengine hata wametembelea mara kadhaa, lakini kimsingi kinachoendelea ni kilekile, hakuna kikubwa tunachoiga na kujifunza, na sababu kubwa ni kuwa hatufanyi juhudi za kujifunza, na hata hatuweki mazingira hayo. Naweza kutoa mifano kadhaa ambayo hata ninapoongea na wachina marafiki zangu huwa wananiuliza.
Ninachokiona hapa China ni kuwa wenzetu wakinunua kitu, huwa hawakifurahii tu, huwa wanaangalia kitu hiki kikoje, kina nini ndani yake, na kinafanya kazi vipi. Maana yake ni kuwa wanataka kujua ni vipi wanaweza kutengeneza kitu hicho, au hata kupata teknolojia yake, ili kesho wasirudi kulekule. Ukiangalia sisi Tanzania unaweza kuona kuwa hakuna juhudi hata kidogo za kuingiza teknolojia, hata ambazo kwa wenzetu ni ndogo na hazihitaji nguvu nyingi. Inawezekana kuwa tuna sera zinazotaja au kuielekeza serikali kwenye mambo haya, lakini ziko kwenye makaratasi tu.
Nikichukulia mfano wa barabara za nchini mwetu Tanzania, utaona kuwa kuna nyingine zimejengwa na makampuni ya kigeni, tena kulikuwa na watanzania wanashiriki kwenye kazi za ujenzi. Lakini hakukuwa na mpango wowote wa maana kukamata utaalam/teknolojia hizo, kama wachina wafanyavyo. Kwa Tanzania ujenzi wa barabara ni mradi endelevu, kwa hiyo lingekuwa ni jambo la maana sana, kama kungekuwa na utaratibu wa maana wa kuweka mazingira ya kuwa na utaalam/teknolojia hizi, leo tungekuwa tumeweza kujenga barabara nyingi tu. Ukiangalia kampuni zinazotoka Ulaya, mara nyingi huwa zinakuja na wataalamu wachache sana, huenda hawafiki hata kumi. Wengine pesa wanapata kutoka kwa serikali yetu wanajenga barabara na kujipatia faida kubwa. Kungekuwa na mipango ya maana (kama ipo, basi ingekuwa inatekelezwa), tungeweza kuwa na wataalamu 10 au hata 20 wa Tanzania wanaoweza kuchukua nafasi ya hao wageni na barabara zikajengwa.
Leo tuna mradi mkubwa wa kujenga bomba la gesi kutoka kusini kuja Dar es Salaam, gharama yake itakuwa ni zaidi ya dola bilioni mbili za Kimarekani. Tungekuwa wachina, tusingekuwa na haja ya kuagiza kampuni kutoka nje kuja kujenga bomba hili na kugharamia fedha zote hizo. Kama tungekuwa na mipango kama ya wachina kupata teknolojia wanazohitaji, ujenzi wa bomba la mafuta kati ya Tanzania na Zambia (TAZAMA) ungekuwa ni funzo ambalo lingetufanya leo tusigharamie mabilioni ya dola kujenga bomba linalofanana na jingine ambalo limewahi kujengwa Tanzania.
Sitaki kuamini kuwa katika mwaka huu na karne hii hatuna watanzania wanaoweza kufanya mambo haya, sitaki kuamini kuwa hatuwezi kuwa na idara ya kuhifadhi teknolojia ambazo tutaendelea kuzihitaji kesho na hata baada ya miaka 100 ijayo. Ni vizuri tujifunze kutoka kwa wenzetu wachina, ili na sisi tuweze kuwa na maendeleo kama wao. Utaratibu wa kuwasifia tu kila siku, wakati sisi hatufanyi juhudi, hauna tija hata kidogo!
Uzuri ni kwamba China ni rafiki mkubwa sana wa Tanzania. Kutokana msingi wa uhusiano wa nchi zetu uliojengwa na mwenyekiti Mao Zedong na Mwalimu Nyeyere, na uhusiano wa karibu kati ya Waziri Mkuu Zhou Enlai na Mzee Salim Ahmed Salim (wakati China iko kwenye harakati ya kupata kiti chake kwenye Umoja wa Mataifa), China iko tayari kutusaidia wakati wowote. Hata leo tukitaka kuomba msaada wa fedha kwa China tunaweza kupewa tena kwa masharti nafuu sana, lakini Je, ni kweli sisi ni watu wa kuomba msaada wa fedha tu kila siku? Hakuna kitu kingine cha kuomba ambacho kinaweza kutusaidia tusiende kuomba tena kesho na chenye thamani kubwa kuliko pesa? Kwanini tuisombe msaada wa teknolojia, ambazo China inazo nyingi na iko tayari kutupatia?
Hata siku moja China haiwezi kusema chukueni teknolojia hii, ina manufaa zaidi kuliko fedha mnazoomba. Utaratibu wa kuomba msaada wa fedha kila siku, na kuomba misaada ya mtindo wa “mkono uende kinywani” (si kutoka kwa wachina tu hata kutoka Ulaya na sehemu nyingine) ni aibu! Ni sawa mtu unapoenda kuomba pesa kwa mtu fulani, hujui ukiondoka nyuma yako mtu huyu atasema nini na atakusemaje mbele ya wengine, na hata ukienda kwake kesho atasema huyu mtu hakuna la maana linalomleta hapa zaidi ya kuomba pesa.
Kwa sasa kuna watanzania wengi sana wanakuja kusoma hapa China, lakini ukiangalia wanachofanya wanaporudi nyumbani ni kama wanamwagwa tu kwenye soko la ajira, na kuingia kwenye mambo ambayo huenda hayana manufaa makubwa. Kama serikali ingewatumia watu hao kisawasawa, huenda leo tungekuwa na kampuni kubwa ya kitanzania yenye uwezo wa kujenga barabara za kiwango cha juu, na hata ambayo ingeweza kupata kandarasi nje ya Tanzania. Lakini kwa sasa bado hatuna “coordinated efforts” za kunufaika.
Kama tukiendea na hali hii tutaendelea kutumia pesa nyingi kufanya yale ambayo tunaweza kuyafanya kwa robo ya gharama. Ni wakati wa viongozi wetu Tanzania kubadilika, kwa manufaa ya watanzania na vizazi vyetu vijavyo!